Kumbikumbi kitoweo, huvunwa msimu wa mvua kuliwa, kuuzwa

Taifa Leo - - UFUGAJI - Na CHRIS ADUNGO

MAMBO mengi yalimshangaza sana Ana Wangare alipofika Emmutete-bunyore katika Kaunti ya Vihiga wiki iliyopita. Karibu na barabara – njia ya kuingia Shule ya Bunyore Girls, aliwaona akina mama na watoto wakiwa wameinama wakiokota kumbikumbi na kuwarusha vinywani.

Kuona wakitafuna wadudu wale, Ana alihisi kichefuchefu nusura atapike. Alishangaa si haba lakini mwenyeji wake, Sara Andoi akamwambia asistaajabu sana kwa vile ile ilikuwa hali ya kawaida katika janibu zile.

Kufika Luanda mjini, aliwaona akina mama wengi wakiwa wanawauzia wateja wao kwenye teo kumbikumbi waliokaushwa kwa wingi. Nao wateja walikuwa wamefurahi kwelikweli.

Si Bunyore tu kunakotegwa kumbikumbi, bali maeneo mengi ya Mkoa wa Magharibi na Nyanza kwa jumla ingawa njia za kuwatega wadudu hao zinatofautiana kidogo. Na kwa yule ambaye pengine hajui kumbikumbi ni wadudu wa aina gani, itakuwa rahisi sana kwake kuelewa.

Kwa Kiluyha wanaitwa Chiswa kwa Kikuyu wanaitwa Nguya na kwa Kijaluo wanaitwa Ngw’en ilhali kwa Kikamba wanaitwa Mbaa.

Kwa mujibu wa Bw James Makate ambaye ni mtaalamu wa wadudu Mkoani Magharibi, kumbikumbi na mchwa ni wadudu wa jamii moja. Huota mbawa na kuruka mvua ikinyesha. Anasema kuna aina mbalimbali za mchwa na hugawanywa kulingana na kazi wanazofanya. Wale ambao hutengeneza vichuguu (nyumba) ni wafanyakazi yaani ‘Workers’. Naye malkia huishi katika kichuguu na hulindwa na askari (Soldiers), ambao ni mchwa wenye vichwa vikubwa.

Aidha anaeleza kuwa kuna misimu miwili ya kupatikana kwa kumbikumbi katika Mkoa wa Magharibi, nayo ni Februari mpaka Aprili kisha Agosti hadi Oktoba.

Ingawa tabia ya kula kumbikumbi huwa kimako kikubwa kwa wageni wanaofika katika Mikoa ya Magharibi na Nyanza, wanaozuru sehemu hizo huzoea pindi wanapoendelea kuishi huko. Kwa mfano, Rosemary Njeri aliyeolewa Bunyore miaka saba iliyopita anasema sasa anajua kuunda mitego ya kuwanasa kumbikumbi na utakuwa unamkosea haki yake iwapo utamnyima mlo wa kumbikumbi waliokaushwa. Ama kweli, chambilecho wazungu ‘ukienda Roma tenda wanavyotenda wao!’

Japokuwa utegaji wa kumbikumbi ni fani ya tangu jadi Mkoani Magharibi, si watu wote wanaoishi huko wanaojivunia utaalamu wa kuunda mitego ya kuwanasa kumbikumbi kama anavyoelezea Tobias Ochua kutoka Ebukanga –Bunyore.

“Kuna watu wengine walio na

Eshibindi, yaani kisirani, nuksi au mikosi. Watu kama hao hata wakiunda mitego mingi kiasi gani, tunawafukuza wakipita karibu na mitego yetu,” akasema Bw Ochua ambaye hunasa hata debe zima la kumbikumbi katika msimu mmoja.

Hata hivyo, wanaouza kumbikumbi kwa wingi ni akina mama. Mkebe mdogo robo-kilo hunadiwa kwa kima cha Sh40 na unaweza kuwapata katika masoko mengi kama vile Luanda, Busia, Lumakanda, Kibunge-kisumu na hata Gikomba, Nairobi.

Lakini kinachowasumbua wengi akili ni jinsi mitego ya kuwanasa kumbikumbi inavyoundwa. “Ni rahisi sana,” akatanguliza Ochua. “Unahitaji tu kutafuta vijiti vingi virefu. Ni lazima viwe vinaweza kukunjika kwa urahisi na itabidi uwe na kamba za kuviunganishia. Utavidungia vijiti hivyo ardhini kisha uzungushe mahali penye kichunguu.

Ni kama utakuwa umeunda kitu mfano wa nyumba ya kuzuilia kuku. Kisha utafunika juu kwa mablanketi na magamba ya migomba na kisha uwache nafasi ndogo ya kuweka karatasi ya nailoni ya kuingiza mwangaza ndani.” Akaeleza.

Ochua anasema mtegaji hulazimika kufyeka nyasi kwenye kichunguu na kumwaga maji kama ndoo saba hivi. Kisha hugongagonga na mawe hapo huku akiimba wimbo wa kitamaduni na kucheza. Inaaminika kuwa hii huwa moja kati ya njia mwafaka za kutolea tambiko mizimu wa kumbikumbi na imetumika tangu zamani miongoni mwa wakazi wa kale katika janibu za Magharibi na Nyanza.

Aghalabu tambiko kama hili hutolewa nyakati za alfajiri na ifikapo asubuhi, kumbikumbi hutika mashimoni wakiingia mtegoni. Hivyo, Mkoani Magharibi; hasa katika maeneo ya Bungoma, Busia na Kitale, watoto wasichana wanaozaliwa msimu wa kumbikumbi huitwa Naswa ilhali wavulana huitwa Waswa. Haya ni kwa mujibu wa Bw Ochua!

“Kuna misimu miwili ya kupatikana kwa kumbikumbi katika Mkoa wa Magharibi, nayo ni Februari -Aprili kisha Agosti Oktoba” -Bw James Makate

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.