Muuguzi akuza ‘pepino melon’ zao lililo na manufaa ya kiafya

Bi Wekesa na mumewe wasema mmea huwapa riziki, afya mbali na kuwawezesha kulipia watoto wao wawili karo shuleni

Taifa Leo - - UFUGAJI - Na PETER CHANGTOEK

VICTOR Agisa na mkewe Lorna Wekesa walipojitosa katika ukuzaji wa mitunda aina ya ‘pepino melon’ miaka kadhaa iliyopita, katika eneo la Sotik, Kaunti ya Bomet, ni wakazi wachache eneo hilo walikuwa na ufahamu kuhusu zaraa hiyo.

Bi Wekesa, ambaye ni muuguzi katika Kituo cha Afya cha Sotik, alikata kauli kujitosa katika shughuli ya ukuzaji wa mimea hiyo, baada ya kuzipata habari za kina kutoka kwa mtaalamu wa lishe, kuhusu manufaa ya matunda hayo kwa afya kwa binadamu.

Mwanzoni, aliikuza mimea hiyo kwa ajili ya matumizi yao wenyewe. Hata hivyo, aliamua kuongeza idadi ya mimea hiyo baadaye.

Mche mmoja, asema, ulimgharimu Sh350, na maadamu aliinunua miche miwili, alishurutika kulipa Sh700. Baadaye, Bi Wekesa alilazimika kuinunua miche mingine 100, kwa kima cha Sh35,000 ili kukiendeleza kilimo hicho kama biashara. Mumewe anasema kwamba ukulima huo huwapa riziki, mbali na kuwasaidia kulipa karo ya shule kwa wanao wawili wadogo.

Walipoona kuongezeka kwa wateja waliokuwa wakiyahitaji matunda hayo, walijifunza jinsi ya kuikuza miche kwa wingi na kuyazalisha matunda hayo kwa wingi. Hata hivyo, waliamua kupunguza bei ya kila mche kuwa Sh150, badala ya Sh350, ili kuwanasa wateja katika eneo hilo.

Wawili hao hukiendeleza kilimo hicho katika shamba ndogo, ambalo ni thumuni ya ekari moja, limilikiwalo na zahanati hiyo. Hata hivyo, anafichua kuwa shamba hilo halitoshi kumzalishia matunda yanayotosha kuwauzia wateja wake.

Kwa wakati huu, aila hiyo huiuza miche pamoja na matunda hayo katika maeneo mbalimbali, mathalan miji ya Bomet, Narok, Kericho, Kisii na Nyamira. Aidha, wao huwapata wanunuzi kupitia kwa baadhi ya maduka makuu kama vile Giftmart, miongoni mwa mengine yaliyoko maeneo ya Kusini mwa Bonde la Ufa na Nyanza.

Changamoto kuu inayowakabili, hata hivyo, ni kutokuwa na shamba kubwa la kulitumia kuyazalisha matunda hayo kwa wingi.

“Tunataka kupanua kilimo na uzalishaji wa matunda, lakini hatuna shamba la kutosha. Tunahitaji kubwa, na tukiipata kampuni ya kushirikiana nayo, nadhani tutayazalisha yanayotosha kuuzwa sokoni,’’ asema Agisa.

Anafichua kuwa wamekuwa wakiyaagiza matunda ya ziada kutoka kwa baadhi ya wakulima ili kukidhi matakwa ya wateja wake. Anaongeza kuwa matunda hayo aina ya ‘Pepino melon’ yanaendelea kutambulika katika eneo hilo polepole, wakati ambapo kuhitajika kwayo kunazidi kuongezeka.

“Matunda hayo, kwa sasa, yanahitajika kwa wingi kwa sababu ya manufaa yayo ya kiafya. Kusini mwa Bonde la Ufa, kwa mfano, matunda hayo yametambulika kwa sababu iyo hiyo,’’ afichua.

Bi Wekesa anasema kwamba mimea hiyo inaweza kukuzwa kwa kuzitumia mbinu mbili; kwa kuzitumia mbegu kutoka kwa matunda yaliyoiva ama kwa kuukata sehemu za mmea huo na kupanda.

“Kwa kuwa wateja wa karibu ni wakulima, tumeamua kuikuza miche ya ziada. Kwa sasa, sisi tunakuza katika kibanda kidogo cha karatasi ya sandarusi. Sisi huzitumia mbegu, lakini matunda ni sharti yakomae ili mbegu ziweze kuonekana,’’ adokeza Bi Wekesa, akiongeza kuwa, wao huuza mche mmoja kwa bei ya Sh150.

Mbali na ukosefu wa shamba la kutosha la kuwawezesha kuiendeleza zaraa hiyo, wawili hao hukabiliwa na changamoto ya magonjwa yanayoiathiri mimea hiyo, pamoja na wadudu waharibifu. Hata hivyo, wao huzitumia dawa kuyakabili magonjwa hayo na kuwaangamiza wadudu hao.

Ili kuusaidia mmea kutoangushwa na matunda hayo, mti wa kuusaidia hutundikwa karibu nao. Mmea huo huyazaa matunda kwa muda wa miezi minne hadi sita kuanzia wakati wa kupandwa kwao.

Agisa asema kuwa baada ya kukomaa kwa mmea huo, matunda yanaweza kuchumwa kila wiki. Anaongeza kwamba mmea huo ukitunzwa ipasavyo, unaweza kuchukua muda wa takriban miaka mitatu kabla haujaangamia.

Bi Wekesa anasema kuwa wao huizalisha miche 1,000 kila baada ya miezi mitatu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.