Je, kilimo hiki kinafaidi makampuni au wakulima maeneo ya mashinani?

Taifa Leo - - UFUGAJI - NA MWANGI MUIRURI

NI miaka 429 ambayo hadi sasa imepita tangu taifa la Kenya liujue na lijihusishe na uchumi wa kilimo cha tumbaku na pia kushiriki soko la bidhaa za kilimo hicho. Lakini kwa miaka hiyo yote, hakuna ushahidi kuwa kuna manufaa halisi ambayo wakulima wa tumbaku hapa nchini wamepata kutokana na uchumi huo.

Kile kilicho wazi ni kuwa makampuni ya kushughulikia biashara za tumbaku ndiyo yamekuwa yakijipa faida nono huku wakulima wenyewe mashinani wakiendelea kuishi katika hali ya umaskini mkuu na kudhoofika kwa afya zao.

Biashara ta tumbaku ilipenyezwa hapa nchini na Wareno mwaka wa 1588 katika eneo la Mombasa ambapo chini ya utawala wa kikoloni waliingiza shehena ya kwanza ya tumbaku katika bandari la Mombasa. Walitia tumbaku katika soko la Kenya pamoja na bidhaa zingine za kilimo kama mihogo na njugu na nyanya.

Lakini tumbaku yenyewe ilikuwa katika soko la dunia kuanzia 3500 BC, huku majani ya mmea huo yakipigiwa debe kuwa na ubora wa kipekee kimatibabu ambapo madaktari wa kienyeji walikuwa wakitumia majani ya mmea wa tumbaku kutibu maumivu ya meno, athari za sumu ya nyoka na kuua wadudu wengine hatari katika afya ya kibinadamu. Sasa, kilimo cha tumbaku na matumizi ya bidhaa za mmea huo za vikiwanda ni masuala mawili ambayo yanaangaziwa pakubwa kuwa na udhalimu wa kiuchumi.

Kilimo cha tumbaku hushamiri katika maeneo ya Bungoma, Busia, Teso Mlima Elgon, Kirinyaga, Murang’a na Thika.

Maeneo mengine ngome ya kilimo hiki ni Meru, Kitui na Machakos sawia na Migori, Kuria, Suba na Homa bay.

Katika kijiji cha Mayanja Kibuke katika Kaunti ya Bungoma ambapo juzi Akilimali ilitembelea kujifahamisha na uchumi huu wa kilimo cha Tumbaku, wenyeji wanateta kuwa “hiki ni kilimo cha utumwa.”

Chifu wa eneo hilo Mathew Juma, anasema kuwa wenyeji wamekuwa katika kilimo hiki cha tumbaku tangu 1976 na hadi sasa hakuna manufaa halisi ya kiuchumi ya kuweka uhakika wazi kuwa ni kilimo cha kibiashara.

“Huwezi ukatumia mmea wa tumbaku kama lishe na katika soko, wakulima wetu hawana lingine ila tu kilio cha mahangaiko ambapo hulipwa malipo duni na kuingizwa katika mikataba ya kiutumwa kuhusu uzalishaji,” asema. Asema: “Ni miaka 41 sasa tangu watu wa hapa waanze kujihusisha na kilimo cha tumbaku. Ni miaka ya umaskini na utumwa.”

Anasema kuwa isipokuwa ni vile taifa limekumbatia mfumo wa utawala wa ugatuzi ambapo kuna serikali za mashinani maeneo mengi ya eneo hilo ambayo hukuza tumbaku hayangekuwea na uwezo wa kushuhudia miundombinu ya kimaendeleo.

“Ni katika kipindi hiki cha ugatuzi ambapo tumeanza kuona maendeleo kama ya mahospitali, mashule na hata zahanati. Kilimo cha tumbaku sio cha faida yoyote kwetu,” asema.

Anasema mashamba ya eneo hilo yamejaliwa rotuba asili na Maulana, “lakini katika kilimo cha tumbaku mashamba haya yamegeuka kuwa sawa na jangwa.”

Anasema kuwa kilimo cha tumbaku pia huathiri uthabiti wa mazingira katika eneo hilo na anasema wakati umefika wa wadau kutafuta njia ya kuwanasua wenyeji kutokana na athari mbovu za kilimo hicho.

Morris Wekesa 58, amekuwa katika kilimo hiki kwa kipindi cha miaka 10 sasa na anakiri kuwa angepata wa kumhami na ujuzi wa kilimo mbadala, atakumbatia mwanya huo bila ya kusita.

Umaskini katika hali hiyo hujiangazia kwa uwazi na ndoa nyingi huyumba kwa kuwa maamuzi ya wazee wa boma ya kuoa wake wasioweza kuwatunza huwa na athari zake,” asema.

Anasema magonjwa ni mengi katika eneo hilo kwa kuwa, “moshi nyingi ambayo hutumika katika kukausha majani hayo ili yawe tayari kwa soko huzua matatizo ya kifua. Dawa ambazo hutumika katika shamba la kilimo cha tumbaku huwa na athari zake na kile tunachopata sokoni huishia kutumika kusaka matibabu.”

Mkurugenzi wa taasisi ya Institute for Natural Resources and Technology Studies (INRS) Samuel Achola anasema kuwa sekta ya tumbaku hapa nchini ni zimwi la kuwaangamiza wakulima wenyewe na pia watumizi wa bidhaa hizo zinazotokana na mmea wa tumbaku.

Anasema kuwa serikali ya Kenya hudinda kuangamiza kilimo hiki kwa kuwa “inavutiwa na ushuru ambao hutokana na sekta hiyo ilihali hesabu za mwisho huonyesha kuwa ushuru huo hata hautoshi kukabiliana na athari za kiafya ambazo huchipuka katika jamii.”

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.