Vikundi: Siri ya kina mama kujiendeleza

Taifa Leo - - UBUNIFU NA BIASHARA - CHARLES WASONGA na LAWRENCE ONGARO

WALIANZA biashara ya kutengeneza na kuuza makaa maalum mnamo mwaka wa 2012 kwa mtaji wa Sh5,000 pekee. Lakini tangu wakati huo, akina mama hawa wamepanua biashara yao kwa kuanzisha mradi ya kufuga ng’ombe wa maziwa na hivi karibuni wanapanga kununua ploti a kujenga nyumba za makazi.

Kufikia sasa kundi hili la Wanawake lililoko katika wadi ya Limuru Mashariki, eneo bunge la Limuru, Kaunti ya Kiambu, lijiimarisha kibiashara kiasi kwamba kufikia sasa linaendesha biashara za thamani ya zaidi Sh600,000

Tunaowazungumzia sio wengine ila kundi la Akina Mama la Karenjee Mwireri lenye wanachama 10 waliojitolea kujiinua kiuchumi badala ya kutegemea waume zao. Aidha, biashara hiyo imewawezesha kuwalipia wanao karo katika shule za upili.

“Sisi hutengeneza makaa haya ya kipekee kutokana na mabaki ya vumbi ya makaa ya kawaida ambayo sisi huchanganya na udongo wa kawaida. Mchanganyiko huo huwekwa maji safi na kukandwa na kuunda umbo la mduara ya saizi mbalimbali. Kisha “mawe” haya hukaushwa kwa muda wa siku kadhaa kulingana na hali ya anga, kabla ya kuuzwa,” anasema Mwenyekiti wa kundi hilo Mama Margaret Wainaina.

Akina mama hao hununua vumbi ya makaa kutokana kwa wafanyabiashara wa makaa katika mji wa Limuru na viungani mwake.

Anasema baada ya “mawe” hayo kukauka wao huyauza kwa wateja wao. Kaa moja ndogo huuzwa kwa Sh5 kila moja ilhali ile kubwa huuzwa kwa Sh10 kila moja.

Akina mama hao hununua mavumbi ya makaa kutokana kwa wafanyabiashara wa makaa katika mji wa Limuru na maeneo ya karibu. Gunia moja la kilo 90 ya mabaki hayo huuzwa kwa Sh300.

“Wananchi wa hapa huyapenda makaa haya kwa sababu hayatoi moshi wenye madhara. Vilevile, ni ya gharama ya chini ikilinganishwa na makataa ya kawaida. Kwa mfano, makaa mawili pekee ya Sh20 yanatosha kupika “githeri” hadi yaive. Kwa upande mwingine, familia ya watu watatu itatumia Sh50 kununua makaa ya kawaida yatakayotosha kuivisha githeri,” anasema Mama Wainaina mwenye umri wa miaka 58.

Anaongeza kuwa makaa hayo pia hupendwa na wakazi wa eneo kwa sababu hutoa joto jingi hasa wakati wa msimu wa baridi. Aidha, Mama Wainaina anasema makaa hayo hununuliwa kwa wingi na wafugaji kuku kwa ajili ya kutoa joto kwa vifaranga ili wakue kwa haraka.

Mama huyo anasema nyakati hizo za kwa wastani, kikundi chake huuza makaa ya thamani ya Sh800.

Lakini wakati wa majira ya baridi hitaji la makaa hayo huwa juu kiasi kwamba wanaweza kuuza jumla ya Sh1,500, ikizingatiwa kuwa eneo la Limuru hushuhudia hali ya baridi kali kuanzia miezi ya Juni hadi Agosti.

“Makataa haya hununuliwa kwa wingi kwa sababu ni salama kutumia na hayana madhara ikilinganishwa na makaa ya kawaida yenye moshi. Bei yetu ya kati ya Sh5 na 10 kwa kaa moja, pia ni nafuu ikilinganishwa na makaa yatokanayo na miti,” anasema kwenye mahojiano na Akilimali wiki iliyopita.

“Tulianza biashara hii kwa mtaji wa Sh5,000 pekee kutokana mpango wetu wa kuweka akiba na kwa ajili ya kujiimarisha kiuchumi yaani, Table Banking. Tunashukuru Mungu kwa sababu sasa tumewaza kuendelea mpaka tukaweza kuwanunua ng’ombe wawili wa maziwa. Aidha, tumemwanzishia Katibu wetu, Bi Felista Wanja, duka la kuuza nafaka (cereals) kwa mtaji wa Sh35,00. Hivi karibuni tutamwanzishia mwanachama mwingine mradi wa Tunapanga kuanzia mwanachama mwingine mradi wa kufuga kuku,” akasema Mwenyekiti huyo.

Anasema ng’ombe hao wawili hutoa jumla ya lita 60 ya maziwa kila siku. Hiyo ina maana kuwa wao hupata takriban Sh3,600 kutokana na mauzo ya maziwa kwa bei ya reja reja ya Sh60 kwa kila lita.

Mama Wanaina anasema mnano Aprili mwaka jana serikali ya kaunti ya Kiambu iliwapa mkopo wa Sh160,000 kwa awamu ya kwanza. Baadaye mwezi Oktoba walipewa mkopo mwingine wa kima cha Sh300,000 ili kupanua biashara yao.

Sasa, akina mama hao wanatoa wito kwa Serikali ya Gavana Ferdinand Waititu Babayao, iwape mikopo mingine ili waweze kuanzisha miradi mingine kama ufugaji kuku, samaki na hata biashara ya nafaka.

“Wanachama wangu wameonyesha ari na bidii katika kazi hii ya kutengeneza makaa na ufugaji ng’ombe wa maziwa. Kwa hivyo, tunaiomba serikali ya sasa ya Kaunti ya Kiambu inayoongozwa na ‘Babayao’ itupatie mikopo zaidi itakayotuwezesha kuanza miradi mingine kama vile ufugaji kuku na samaki. Wengine wetu pia wanataka kufungua kazi ya “cereals” lakini shida ni pesa za mtaji,” akaeleza mwenyekiti huyo.

Wanachama wa kundi hilo wanaitaka serikali ya Gavana Waititu kutuma maafisa wake mahala pao pa kazi ili wakague miradi yao kwa lengo la kuwapiga jeki kwa njia ya kuwapa mikopo ya kujiendeleza.

“Wanachama wangu wameonyesha ari na bidii katika kazi hii ya kutengeneza makaa na ufugaji...” -Mama Wainaina

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.