Changamoto kupata mikopo kiini cha kutofanikisha kilimo

Taifa Leo - - UBUNIFU NA BIASHARA - Na Ludovick Mbogholi

NYENYE Mwaruwa Chirembe, 29, ni mkulima mwenye bidii katika eneo la Marugube ‘A’ katika kijiji cha Dumbule huko Kinango Kaunti ya Kwale. Mkulima huyu alitumia Sh10,000 katika harakati zake za kuhakikisha ununuzi wa mbegu za mazao ya vyakula , dawa na mbolea zinafaulu.

Aidha, pesa hizo pia alihakikisha zinatumika vyema kwa shughuli za kuweka vibarua kupalilia na hata kuvuna mazao yake. Bwana Chirembe amekuwa akilima miembe , nyanya, biringanya, mabenda na hata kukuza na kustawisha miti ya matunda ya mipera shambani kwake.

Akiongea na Akilimali shambani kwake huko Marugube ‘A’ kijijini Dumbule kaunti ndogo ya Kinango , mkulima huyu anadai anakumbwa na changamoto nyingi za ukulima kama shida ya maji ya kutosheleza kustawisha mazao yake , ukosefu wa mbolea , ukosefu wa dawa na uvamizi wa wadudu waharibifu. Hata hivyo, anadai kuwa shida kubwa inayompa changamoto si haba ni ukosefu wa fedha za kutosha kuendeleza ukulima wa kisasa.

Mbali na matatizo yanayomlemea bwana Nyenye Mwaruwa Chirembe , anajitahidi kuvuta maji kidogo kutoka kwenye mto mdogo ulioko umbali wa mita 500 kutoka kwenye minazi. Anasikitika kuwa shida ya kupata mikopo kutoka kwa mashirika husika inamkwaza mno katika maendeleo ya kilimo akijielewa kuwa kilimo ndicho mwajiri maishani mwake.

Anafichua pia kuwa kuna usumbufu mwingi wa mifugo wanaoharibu mazao yake shambani hali inayomlazimu mara nyingi kukeshea humo. Fauka ya hayo yote , mkulima huyu anasema zao la biringanya hukua na kuhitimu kwa muda wa miezi miwili kabla ya mavuno huku zao la mabenda likichukua mwezi mmoja pekee kabla ya kukomaa na kuvunwa.

Kwa sasa, Bw Chirembe anasema zao lake la biringanya lina umri wa nusu mwezi pekee kabla ya kukomaa kwa mavuno huku mabenda yakiwa tayari kwa kuvunwa.

Anaambia Akilimali kuwa baada ya kuvuna mazao yake , anawapelekea wachuuzi wadogowadogo mitaani huku wengine wakimjia shambani kujinunulia.

Hata hivyo, anadokeza kuwa nyanya anazokuza sasa zina mwezi mmoja pekee na imesalia miezi miwili zaidi ndipo zivunwe.

Bwana Nyenye anasema shamba lake lenye ukubwa wa ekari 5 ndilo shina na msingi thabiti wa maisha yake kwani analitegemea sana kukidhi majukumu na maslahi muhimu ya familia yake changa. Anasema kuwa kila msimu wa ukulima anatumia pesa nyingi kwenye palizi na hata kwa malipo ya vibarua wanaomsaidia wakati wa mavuno. Hata hivyo anakiri kuwa anapata pato si haba kwani kwa kila msimu anaweza kujiingizia faida ya Sh20,000!

Kadhalika mkulima huyu anafichulia Akilimali kuwa katika miaka yake yote ya ukulima , amekuwa akitarajia wateja wa jumla na rejareja ila shida kubwa inayomtia kiwewe ni ukosefu wa soko au masoko ya kuuzia mazao yake. Kutokana na hali hiyo anajukumika kufanya biashara ya kuuza mazao shambani badala ya kusafiri umbali wa kilomita 22 hadi mjini Kinango.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.