Bei ya majanichai jijini Mombasa yapanda

Wanunuzi bidhaa hii wameongezeka kutokana na hofu ya biashara kudorora katika kura ijayo

Taifa Leo - - RIZIKI HABARI ZA KILIMO NA BIASHARA - FAUSTINE NGILA

BEI ya majanichai katika soko la Mombasa ilipanda kwa kiwango cha juu zaidi katika kipindi cha miezi saba iliyopita hapo Jumanne.

Hii ni baada ya wanunuzi kununua bidhaa hiyo kwa wingi kutokana na hofu kuwa biashara itasambaratishwa na marudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 26.

Takwimu kutoka shirika la Muungano wa Wafanyabiashara wa Majanichai Afrika Mashariki (EATTA), zinaonyesha kuwa kilo moja ya majanichai iliuzwa kwa Sh310 kwa wastani wiki hii kutoka Sh297 wiki iliyopita, ambayo ndiyo bei ya juu zaidi tangu mwezi Februari.

“Bei ya wastani imekuwa nzuri sana na ni ishara kuwa kila mfanyabiashara analenga kuwa na majanichai ya kutosha,” akasema meneja mkurugenzi wa muungano huo Bw Edward Mudibo.

Wafanyabiashara wamesema kuwa bei ya bidhaa hiyo inatarajiwa kuwa Sh300 kwa kilo katika mwezi mmoja ujao wakati Wakenya wanajitayarisha kurudi debeni kuchagua rais.

Shirika hilo limesema ongezeko la bei limechangiwa pakubwa na ununuzi wa hofu huku suitafahamu ikikumba uchumi kutokana na shaka ya matokeo ya marudio ya uchaguzi wa urais. Bw Mudibo alifichua kwamba wafanyabiashara wengi wameuza zao lao kwa zaidi ya Sh400 kwa kilo, hali ambayo imeboresha bei ya wastani ya bidhaa hiyo katika soko la

Mombasa.

Soko hilo ni jungu la kanda ya Afrika Mashariki katika biashara ya majanichai, huku mataifa zaidi ya 19 barani Afrika yakiuza mazao yao katika soko hilo.

Kila aina ya majanichai huuzwa kwa bei tofauti kulingana na ubora wake.

Hapo Jumanne, kilo 8.88 milioni za majanichai zilifikishwa katika soko hilo tayari kwa mauzo, na ambapo kilo milioni 8.081 za bidhaa hiyo ziliuzwa huku kilo chini ya milioni moja zikisalia kutouzwa.

Taifa la Pakistan liliongoza katika ununuzi huku Yemen na mataifa mengine ya Mashariki ya Kati pia yakionyesha uwezo wake wa kununua.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.