Wanajeshi 17 wauawa na Al -Shabaab katika shambulio kambini

Taifa Leo - - HABARI ZA AFRIKA NA DUNIA -

WANAMGAMBO wa al-shabaab walishambulia kambi ya kijeshi nje ya mji mkuu wa Mogadishu kwa kutumia gari la mabomu na bunduki.

Wanajeshi 17 waliuawa katika shambulio hilo, kabla ya wanamgambo hao kutwaa kambi hiyo na kijiji cha karibu.

Ripoti hii ni kwa mujibu wa kundi hilo Ijumaa.

Wakazi na maafisa wa serikali walithibitisha shambulio hilo lakini hawakutoa habari zozote kuhusiana na majeruhi au vifo.

“Baada ya maombi ya asubuhi leo, wapiganaji wawili walivamia kambi ya Barire wakiwa na gari la mabomu. Tuliua wanajeshi 17 na kutwaa magari saba ya kiufundi,” alisema Abdiasis Abu Musab, msemaji wa operesheni wa al-shabaab katika mahojiano na Reuters.

Magari ya kiufundi yaliyotwaliwa ni yale ya kubeba bunduki atomatiki.

“Wanajeshi wengine walikimbia na kujificha, sasa tumedhibiti kambi hiyo na kijiji kilicho karibu,” aliongeza.

Barire ni kilomita 50 kusini magharibi mwa Mogadishu.

Al Shabaab inalenga kutwaa serikali ya Somalia ili kukalia wananchi kwa kutumia sheria kali zaidi za Kiislamu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.