Ingwe, Sofapaka kuchapana Narok

Taifa Leo - - SPOTI - Na JOHN ASHIHUNDU

MABINGWA wa zamani, Sofapaka FC na AFC Leopards watasafiri hadi Kaunti ya Narok kupambana katika mechi ya Ligi Kuu inayodhaminiwa na Sportpesa.

Leo, vinara wa ligi hiyo, Gor Mahia watakuwa mjini Kisumu kuvaana na Bandari ugani Moi Stadium wakitafuta ushindi wa kuwawezesha kuendelea na uongozi kwa pengo kubwa.

Mjini Narok, Sofapaka ambao waliichapa Ingwe 1-0 katika mkondo wa kwanza watakuwa wakitafuta kuendeleza ubabe wao mbele ya mabingwa hao mara 13.

Ushindi kwa vyovyote vile

Sofapaka, mabingwa wa 2009 wanatafuta ushindi kwa vyovyote vile baada ya kuendelea kupata matokeo ya kuchanganya katika mechi za hivi karibuni.

Mbali na majeraha kuwa tatizo kwa baadhi ya nyota wao wa kutegemewa, kuondolewa kwa Zoo Kericho na Nakumatt kumesababisha kupokonywa kwa mabingwa hao wa zamani pointi sita.

Hatua hiyo amefanya wapoteze nafasi ya pili na kushuka hadi nafasi ya nne.

Zoo na Nakumatt zimeondolewa nje baada ya mahakama kuu kuamua timu za ligi hiyo zibakie 16.

Timu hizo zinasubiri uamuzi wa kesi ya rufaa iliyowasilishwa mahakamani na Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kupinga uamuzi huo.

Kwa mara nyingine, Sofapaka watamtegemea mshambuliaji tegemeo, Umaru Kasumba raia wa Uganda ambaye anakamata nafasi ya pili kwa ufungaji mabao nyuma ya Stephen Waruru kwa tofauti ya bao moja.

Kipa chaguo la kwanza, Mathias Kigonya pia amerejea baada ya kuwa nje kwa siku kadhaa kutokana na jeraha.

“Hii ni mechi ngumu, lakini lazima tushinde. Tumetatizika katika mechi za hivi karibuni, lakini nina matumaini tutarejea katika hali yetu njema na kuanza kupata ushindi,” alisema kocha wao, Sam Ssimbwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.