Arsenal yatesa makinda wa Europa League

Taifa Leo - - SPOTI -

ARSENAL iliendelea kutesa katika Ligi ya Uropa baada ya kunyamazisha wenyeji BATE Borisov 4-2, huku Everton ikijikwaa 2-2 dhidi ya wageni Apollon Limassol mnamo Alhamisi.

Olivier Giroud alifikisha mabao 100 akivalia jezi ya Arsenal. Viongozi wa kundi H, Arsenal, ambao walitumia chipukizi wengi dhidi ya Borisov, walipata ushindi kupitia mabao ya Theo Walcott (mawili), Rob Holding na Giroud.

Arsenal ya kocha Arsene Wenger ina jumla ya pointi sita. Ilipepeta Cologne 3-1 uwanjani Emirates wiki mbili zilizopita.

Wenger alifanya mabadiliko tisa katika kikosi kilichozaba West Bromwich Albion 2-0 katika Ligi Kuu hapo Jumatatu.

Wachezaji Shkodran Mustafi na Mohamed Elneny walihifadhi nafasi zao, huku chipukizi kadhaa wakionja mashindano haya ya daraja la pili ya Bara Ulaya akiwemo Joe Willock, 18, aliyepata namba katika kikosi cha watu wazima kwa mara ya kwanza kabisa. Borisov ilifuta machozi kupitia mabao ya Mirko Ivanic na Mikhail Gordeichuk. Cologne ilidhalilishwa tena ilipoaibishwa 1-0 nyumbani nchini Ujerumani na Red Star Belgrade kutoka Serbia.

Nayo Everton ilisalia bila ushindi katika kundi E baada ya kuachilia uongozi uwanjani Goodison Park. Apollon ilitangulia kuona lango kupitia Adrian Sardinero dakika ya 12 kabla ya Wayne Rooney na Nikola Vlasic, ambaye aliingia kama mchezaji wa akiba, kuweka Everton 2-1 juu.

Hata hivyo, Everton ilizembea Apollon iliposalia watu 10 uwanjani baada ya Valentin Roberge kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 86 na kuadhibiwa. Hector Yuste alisawazisha 2-2 kupitia kichwa kisafi dakika ya 88 Apollon ilipopata ikabu.

Everton inavuta mkia kwa alama moja. Viongozi Atalanta wana pointi nne. Walitoka sare ya 1-1 dhidi ya Lyon nchini Ufaransa.

Naye Patrick Cutrone aliinasua wenyeji AC Milan kutoka minyororo ya kudondosha alama alipofunga bao lililozamisha Rijeka ya Croatia 3-2 sekunde za mwisho katika mechi ya Kundi D uwanjani San Siro.

Matokeo mengine ni Marseille 1-0 Salzburg, Athletic Bilbao 0-1 Zorya Luhansk, Hertha Berlin 0-1 Ostersund, Lokomotiv Moscow 3-0 Zlin, Nice 3-0 Vitesse Arnhem nao mabingwa wa zamani Zenit St Petersburg wakalipua Real Sociedad 3-1.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.