UTEUZI WA KARUGU KAMA NAIBU GAVANA WAINUA NAFASI YA MWANAMKE

Bi Karugu ndiye mwanamke wa 2 kushikilia nafasi hiyo eneo hilo, baada ya Bi Mbuthia wa Nyandarua

Taifa Leo - - Front Page - Na WANDERI KAMAU

KUTEULIWA kwa Bi Carol Karugu kama Naibu Gavana wa Kaunti ya Nyeri kumeongeza usemi wa mwanamke katika siasa za ukanda wa Mlima Kenya, wengi wakionekana kuwapiku wanasiasa wanaume.

Kwa sasa, Bi Karugu ndiye mwanamke wa pili kushikilia nafasi hiyo katika ukanda huo, baada ya Bi Cecilia Mbuthia, ambaye ni Naibu Gavana katika Kaunti ya Nyandarua.

Bi Karugu alipendekezwa wiki iliyopita na Gavana Mutahi Kahiga kama naibu wake, baada ya kifo cha mtangulizi wake, Dkt Wahome Gakuru.

Tangu Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8 mwaka uliopita, wanawake wengi wamejitokeza kama viongozi wakakamavu wa kisiasa, huku nyota zao za kisiasa ziking’aa kila kuchao.

Baadhi yao ni Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, kiongozi Narc-kenya Martha Karua, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Kiambu Gathoni wa Mumbomba, Bi

Wangui Ngirichi (Kirinyaga), Bi Sabina Chege (Murang’a), wabunge Alice Wahome (Kandara), Martha Wangare (Gilgil) kati ya wengine.

Wachanganuzi wa masuala ya uongozi wanasema kuwa huenda mkondo huo ukaashiria “ukombozi mpya wa mwanamke” kama ilivyoshuhudiwa wakati wa Bi Wangu wa Makeri, kiongozi mwanamke katika jamii ya Agikuyu ambaye aliwakabili vikali wanaume.

“Ni ishara kwamba wanawake wameanza kujikomboa kisiasa, baada ya siasa za eneo hilo kudhibitiwa sana na uongozi wa wanawake kwa miaka mingi,” asema Bi Judy

Mwangi, ambaye ni mtalamu wa masuala ya uongozi katika Chuo Kikuu cha Mt Kenya.

Kwa kipindi kidogo ambacho Bi Waiguru amehudumu kama gavana, ameweza kuteuliwa kama Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (COG).

Zaidi ya hayo, ndiye mwenyekiti wa kamati andalizi ya Kongamano la Ugatuzi ambalo linatarajiwa kufanyika katika Kaunti ya Kakamega wiki ijayo.

Bi Waiguru pia alihudumu kama Waziri wa Ugatuzi, katika kipindi cha kwanza cha serikali ya Jubilee, ambapo wizara hiyo ilishughulikia masuala muhimu kama utaratibu

wa ugavi fedha kwa serikali za kaunti. Bi Mwangi anataja hilo kama ishara ya uwezo mkubwa wa uongozi alio nao Bi Waiguru.

“Uteuzi wake kama naibu mwenyekiti wa COG unaashiria imani kubwa ambayo magavana wenzake walio nayo kwake. Hii ni kwa kuwa yeye ni mwanamke wa kwanza kushikilia nafasi hiyo,” asema Bi Mwangi.

Kwa upande wake, Bi Karua amejitokeza kuwa asiyetetereka kisiasa, kwani angali anashikilia kwamba uchaguzi wa ugavana katika kaunti ya Kirinyaga haukuendeshwa kwa njia huru na haki.

Picha/maktaba

Bi Caroline Wanjiru Karugu akiwa katika mkutano awali mjini Nyeri. Uteuzi wake kama Naibu Gavana wa Nyeri umeinua hadhi na usemi wa mwanamke eneo la Mlima Kenya. Wanawake wengine eneo hilo wamekuwa wakakamavu kisiasa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.