Joho apata wafadhili wa kusafisha maji ya bahari ili yatumike nyumbani

Taifa Leo - - Front Page - MOHAMED AHMED na WINNIE ATIENO

TATIZO la uhaba wa maji katika kaunti ya Mombasa linatarajiwa kumalizika kabisa, kupitia mbinu mpya ya kusafisha maji ya bahari. Mpango huo unaotarajiwa kuwa wa kwanza kutekelezwa Afrika Mashariki, umo njiani baada ya Gavana wa Mombasa Hassan Ali Joho kukubaliana na wafadhili.

Bw Joho alikutana na wadau wa Uhispania ambao wanapanga kuanzisha mradi wa kubadilisha maji ya bahari kuwa maji safi ya matumizi ya nyumbani. Iwapo mradi huo utafanikiwa, utakuwa ni afueni kubwa kwa zaidi ya wakazi milioni moja wa kaunti hiyo ya Pwani, ambao wanaendelea kukabiliwa na tatizo sugu la kukosekana maji ya kutosha. Serikali hiyo ya Mombasa tayari ilikuwa imetoa zabuni kwa kampuni ya kutoka Uhispania na Uswizi.

Mradi huo unatazamiwa kuanza baada ya mwezi mmoja. Bw Joho alisema kuwa mkutano ambao umefanyika baina yake na katibu wa wizara ya kilimo na mazingira ya serikali ya Uispania utazaa matunda.

“Mradi huu utaweza kutoa mita mche 100,000 na utatuwezesha kutoa maji kwa wakazi wetu bila shida yoyote. Tutaweza kuwa na maji ya kutosha kwa matumizi yetu ya kila siku,” akasema Bw Joho kupitia mtandao wake wa Facebook.

Kulingana na waziri wa Maji wa kaunti hiyo, Bi Fatma Awale ambaye pia ameandamana na Bw Joho katika safari hiyo nchini Uhispania, serikali ya kaunti itaweka viwanda viwili vya kubadilisha maji hayo ya bahari.

Alisema kuwa kiwanda kimoja kikubwa kitakuwa upande wa Kisauni na kitajengwa kwa muda wa miezi 15 na kingine kidogo kitachukua miezi 12 na kitakuwa upande wa Likoni.

“Kama kaunti tunahitaji mita mche 180, 000 kwa siku lakini kwa sasa tunapokea mita mche 43, 000 pekee ambazo hazitoshi. Lakini muda tutakuwa na viwanda vyetu vya kubadili maji haya basi tatizo hili litasahaulika,” akasema Bi Awale.

Aidha kwa sasa, Bi Awale alisema kuwa wamekuwa wakipambana na shida ya wizi wa maji unatokelezwa na watu wanaoiba kupitia mabomba ya maji.

Alisema kuwa watu hao wamekuwa wakiendesha biashara hiyo kinyume cha sheria na kaunti imeanza msako dhidi yao.

Watu hawa ndio wanachangia shida ambazo wakazi wetu wanapata kwani sehemu nyengine hazipati maji hata yale kidogo wanayopaswa kupata. Lazima tupambane na watu hao huku tukifafuta suluhu ya kudumu,” akasema Bi Awale.

Picha/maktaba

Gavana Joho(kulia) akiwa na viongozi wengine wa Mombasa katika hafla ya awali eneo hilo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.