Wamalwa ataka daraja la Kainuk lirekebishwe upesi

Waziri ataja daraja hilo kuwa muhimu katika uchumi

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - Na SAMMY LUTTA

WAZIRI wa Ugatuzi, Bw Eugene Wamalwa, amemwambia mwenzake wa uchukuzi, Bw James Macharia, aharakishe kujenga daraja la Kainuk katika mpaka wa Kaunti za Turkana na Pokot Magharibi ili kurahisisha usafiri wa watu na mizigo.

Bw Wamalwa ambaye alizuru daraja hilo Ijumaa alipokuwa akikagua athari za mafuriko na hali ya njaa katika kaunti hiyo alijionea malori mawili ambayo yalisombwa na maji yalipokuwa yakielekea Lodwar.

Alisema usafiri umekwama na hali inazidi kuwa mbaya kwani mvua kubwa inazidi kunyesha katika eneo hilo.

“Daraja la Kainuk ni muundomsingi muhimu katika barabara ya Kitale kuelekea Lodwar, na usafirishaji wa chakula cha msaada pia huathirika kila wakati daraja hilo linapojaa maji,” akasema waziri.

Alisema serikali itawekeza katika ujenzi wa mabwawa makubwa ili kudhibiti mafuriko katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Bw Wamalwa ambaye aliandamana na Katibu wa Wizara anayesimamia Ardhi Kavu, Bw Michael Powon, alisema serikali kuu imejitolea kuwezesha maeneo kame nchini yakome kutegemea usambazaji wa vyakula vya

msaada.

Waziri alipokewa na Gavana wa Turkana, Bw Josphat Nanok, Kamishna wa Kaunti Seif Matata, Mbunge wa Turkana Kusini James Lomenen na kamati ya usimamizi wa kaunti katika makao makuu ya kaunti mjini Lodwar.

Bw Nanok alisema serikali ya kaunti itashirikiana na serikali kuu kutafuta suluhisho ya kudumu ili kukabiliana na athari za uhaba wa mvua, ukame, mafuriko yanayotokea wakati wa msimu wa mvua na uhaba wa vyakula.

Picha/kanyiri Wahito

Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa katika mkutano Januari 31, 2018. Alizuru daraja la Kainuk lililoathiriwa na mafuriko na akataka wizara ya Muundomsingi ilirekebishe upesi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.