Wavalia njuga kampeni ya usafi wa mdomoni mashinani

NYOTA NDOGO

Taifa Leo - - Front Page - NA PAULINE ONGAJI

Utafiti uliofanywa miaka mitatu iliyopita na shirika la kitaifa linalohusika na afya ya mdomoni nchini Kenya National Oral Health, uwiano baina ya idadi ya madaktari wa meno na idadi ya raia hapa Kenya ni 1: 42000.

Takwimu hizi zinaonyesha kuwa kila daktari mmoja wa meno ana jukumu la kushughulikia wagonjwa 42,000, tofauti na mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya daktari mmoja kwa kila wagonjwa 7,000.

Isitoshe, ripoti hiyo ilionyesha kwamba wengi wa wataalam hawa wako katika maeneo ya miji, suala linalowanyima wakazi wa maeneo ya mashambani fursa ya kupokea huduma hii.

Ni sababu hii iliyowachochea Erick Ocholla 27 na Vincent Omondi, 27, wataalam wa meno, kutaka kubadilisha taswira hii ambapo kupitia shirika waliloanzisha la Oracare wamekuwa wakihamasisha jamii kuhusiana na umuhimu wa kudumisha usafi wa mdomoni.

Huu ukiwa mwaka wao wa pili tangu kuanzisha mradi huu, maelfu ya Wakenya wamenufaika na huduma zao ambapo wamekuwa wakitembelea shule za msingi huku wakimakinika na maeneo yanayokabiliwa na umaskini.

“Kwa ushirikiano na Muungano wa kitaifa wa madaktari wa watoto na kampuni ya Pepsodent, tumetembelea shule za msingi za Mwiki, Athi River, Umoja Pipeline, Rongai, Kawangware, Ngong na Victoria katika Kaunti ya Kisumu,” aeleza Bw Omondi.

Anasema kwamba nia yao ya kulenga watoto hasa kutoka maeneo maskini ni kutokana na sababu kuwa katika sehemu hizi wakazi hawana muda wala rasilmali za kushughulikia suala hili.

Shughuli zao hazihusishi tu wanafunzi kwani pia wamekuwa wakipeleka kampeni hizi katika vituo vya kijamii na maeneo ya ajira. “Baadhi ya kampuni ambazo tumetembelea kutoa huduma hizi ni pamoja na matawi kadha ya Benki ya KCB, shirika la Rift Valley Railways na NSSF Kisumu miongoni mwa mengine,” aeleza Bw Ocholla.

Kwa hivyo kila mara wana kikosi kinachotembelea sehemu tofauti kutafuta fursa ya kuandaa kampeni hizi.

Shughuli zao zimekuwa kufanyia watu uchunguzi wa meno na kutambua matatizo yanayowakumba, bali na kutoa bidhaa za kudumisha usafi wa mdomoni kama vile miswaki na dawa ya meno.

“Tumekuwa tukishirikiana na kampuni za kuunda dawa ya meno kusambaza bidhaa hizi. Mwaka jana tulishirikiana na kampuni ya Colgate, ambapo maelfu ya watoto walielimishwa kuhusu jinsi ya kudumisha usafi wa mdomoni. Kadhalika kwa ushirikiano na kampuni ya kutengeneza dawa ya Glaxosmithkline-gsk, tumekuwa tukiendeleza vikao katika maeneo tofauti,” asema Bw Omondi.

Katika shughuli hii wametambua na kushirikiana na madaktari wa meno kutoka kila kaunti ambapo watu wanaopatikana na maradhi wanatibiwa, huku wengine wakishauriwa kwenda katika hospitali za kitaifa.

“Katika harakati hizi tunaamini kuwa tumekuwa tukizuia kuenea kwa maradhi ya meno hasa ikizingatiwa kuwa tunafanya kazi na madaktari wa meno wanaotoa huduma zao kwa bei nafuu,” aeleza Bw Ocholla.

Ari yao ya kuanzisha huduma hii ilianza baada ya kugundua kuwa suala la afya ya mdomo halikupewa kipaumbele kama lilivyostahili. Hii ilikuwa baada ya wawili hawa kuhitimu kutoka chuo cha mafunzo ya tiba ya meno.

Kwa sasa ndoto yao ni kununua gari lililo na vifaa vyote vinavyohitajika kwa matibabu ya meno n a hivyo kuwasaidia kutoa matibabu kila wanapotembelea maeneo haya.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.