Wanjala nje kwa dhamana kufuatia ghasia

Alikamatwa baada ya wafuasi wake na wa Ababu kukabiliana

Taifa Leo - - Buriani Matiba - Na GAITANO PESSA

MBUNGE wa Budalang’i Raphael Wanjala jana aliachiliwa huru kwa dhamana ya Sh400,000 pesa taslimu na mdhamini wa Sh700,000 baada ya kukamatwa kuhusiana na ghasia zilizotokea katika daraja la Sigiri eneo bunge hilo Ijumaa.

Walipofika mbele ya Hakimu Mkuu wa Busia Martha Nanzushi, mbunge huyo pamoja na watu wengine wanne-mbaga Tuzinde, John Michula, Alfred Wesonga na Peter Otuna- walikana mashtaka dhidi yao.

Walishtakiwa kwa kuhujumu mamlaka ya afisa wa serikali, kuhatarisha usalama wa ndege na abiria wake, kuchochea ghasia na kumzuia afisa huyo kuhutubia umma.

“Mnamo Aprili 13, Bw Wanjala pamoja na wengine ambao hawakuwepo kortini ulihatarisha usalama wa maafisa wa serikali ambao walikuwa kwenye ndege hiyo karibu na daraja la Sigiri eneo bunge la Budalangi, hatua ambayo ilisababisha fujo na kisha wakamzuia afisa wa umma kuhutubia umma,” akasema Jaji Nanzushi.

Hata hivyo, Bw Wanjala kupitia wakili wake Haman Omiti alilalamika kuwa dhamana hiyo ilikuwa ya kiwango cha juu akisema, “hii ina maana kuwa korti inatumiwa kututisha.”

“Tunahisi kwamba dhamana hiyo ni ya juu zaidi ikizingatiwa kuwa baadhi ya washtakiwa ni watu wenye mapato ya chini. Hata mdhamini wa kiasi cha Sh700,000 kila mmoja ni cha juu zaidi. Tunapanga kuwasilisha pingamizi dhidi ya uamuzi huo,” akasema Bw Omiti.

Naye Bw Wanjala akasema: “Nadhani idara ya mahakama na polisi wanatumiwa na watu wengine. Ni haki yetu kutozwa kiwango cha chini cha faini.

“Nilisikia Bw Namwamba alisema amenisamehe. Sijui nimemfanyia kosa gani kiasi cha kunisamehe. Anafaa kukoma kuingilia kazi yangu,” akasema Mbunge huyo wa chama cha ODM. Bw Wanjala alikamatwa mjini Kisumu Jumamosi baada ya kisa ambapo wafuasi wake walikabiliana na wale wa Bw Namwamba ambaye ni Waziri Msaidizi wa Mashauri ya Kigeni.

Makabiliano hayo yalizuka wakati wa zoezi la ukaguzi wa ujenzi daraja hilo la Sigiri na barabara ya Busia kwenda Malaba, shughuli ambayo iliongozwa na Waziri Msaidizi wa Uchukuzi na Miundo Msingi Chri Obure.

Katika patashika hiyo, watu waliodaiwa kuwa wafuasi wa Bw Wanjala waliishambulia kwa mawe helikopta ambayo ilikuwa imewabeba Mabw Obure, Namwamba na Kamishna wa Kaunti ya Busia Michael Tialal.

Kesi hiyo imeratibiwa kusikizwa mnamo Agosti 22 mwaka huu.

Picha/gaitano Pessa

Mbunge wa Budalang’i Raphael Wanjala (kulia) akiwa na washtakiwa wengine kortini, Busia, jana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.