Maafisa waanza msako kukagua vifaa vya afya, wahudumu waliopo

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - Na BRIAN OCHARO

MAAFISA wa afya katika kaunti ya Mombasa wameanzisha uchunguzi katika vituo vyote vya afya kuhakikisha kuna vifaa mwafaka vya matibabu pamoja na wahudumu wa afya waliofuzu kushughulikia wagonjwa inavyohitajika.

Mkurugenzi wa afya Dkt Khadija Shikely alisema maafisa wa afya wanachunguza maabara zote ili kuhakikisha kuwa vifaa vilivyopo vinastahili.

“Tunachunguza maabara zote na hata zile zinazofunguliwa ili tuhakikishe kuwa wanaofanya vipimo wana ujuzi sawia na vifaa kama vinastahili na katika mandhari salama,” alisema.

Dkt Shikely alisema bodi ya matibabu ya meno imeweka afisa katika kaunti hiyo ili kusaidia katika zoezi la kufungwa kwa vituo vyote vya afya na maduka ya dawa ambayo hayajafuata sheria.

Alisema kuwa zoezi hilo litahakikisha kuwa vituo vya afya vinaafikia vigezo vinavyostahili, wahudumu wa afya walio na tajriba na yeyote anayeshughulika na masuala ya dawa awe na ujuzi na uzoefu pamoja na uaminifu kwa wagonjwa.

“Tunachunguza vituo vyote vya afya vya kibinafsi ambavyo vinachipuka, maabara, maduka ya dawa, wauguzi na madaktari, tunataka kujua kama kweli wote ni madaktari au wauguzi waliohitimu,” alisema.

Dkt Shikely alikuwa akizungumza eneo la Mama Ngina Drive wakati wa maadhimisho ya siku ya sayansi ya dawa na mabara duniani.

Zaidi za wakazi 1,000 walijitokeza kupimwa maradhi tofauti tofauti bila malipo kwa udhamini wa watu wanaoshughulikia masuala tofauti katika maabara.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.