Barabara kuu kuwekwa lami kukabili mafuriko

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - Na GEORGE SAYAGIE

SERIKALI ina mpango wa kuweka lami katika barabara ya Kibiko-kimuka-suswa, inayounganisha kaunti za Narok na Kajiado, ili kukabili mafuriko ambayo yamekuwa yakitokea katika eneo hilo kila mara.

Barabara hiyo ina urefu wa kilomita 70.

Gavana Samuel Tunai wa Narok alisema jana kwamba tayari amemwarifu Rais Uhuru Kenyatta, akimwomba msaada kusaidia katika ujenzi wake kupitia Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi wa Barabara (KENHA).

Akizungumza katika mkahawa wa Keerokok Lodge, wakati akizindua mkakati wa usalama wa mpakani kati ya kaunti yake na Tanzania, Bw Tunai alisema kwamba barabara hiyo itakuwa afueni kubwa, hasa kwa waendeshaji magari.

Alisema kuwa itawasaidia kufupisha mwendo wa kufika Kajiado kutoka Narok, hasa wakati hali ya anga inakuwa mbaya.

Kwa sasa, watu wengi ambao wanasafiri Narok kutoka Kajiado ama Nairobi huwa wanalazimika kutumia barabara ya Maimahiu ili kufika kaunti hiyo.

“Ninafanya mashauriano na Rais Kenyatta na Naibu Rais William Ruto ili kuwarai kututengea fedha kwa ujenzi wa barabara hii katika mwaka ujao wa matumizi fedha za serikali ili kukabili matatizo ya usafiri ambayo hutokea wakati wa mvua,” akasema gavana huyo.

Aidha, alitoa mfano wa kuchelewa kwa waendeshaji magari waliokuwa wakielekea Nairobi wakitumia barabara hiyo mnamo wikendi.

Mafuriko mengi ambayo yamekuwa yakiendelea katika eneo hilo yalikatiza usafiti katika eneo la Suswa, baada yake kukatika vipande viwili.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.