Benki zilifuta 1,62O mwaka uliopita - Ripoti

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - Na VALENTINE OBARA

WAFANYAKAZI zaidi ya 1,620 wa benki nchini walisimamishwa kazi katika mwaka mmoja uliopita, ripoti imeonyesha.

Ripoti hiyo ya shirika la Cytonn Investments ambayo ilitolewa Jumapili ilisema wafanyakazi hao walisimamishwa kazi baada ya benki mbalimbali kufunga matawi kadhaa katika pembe tofauti za nchi.

Miongoni mwa benki ambazo zilifichua idadi ya wafanyakazi waliofutwa kazi, Benki ya Equity iliongoza kwa wafanyakazi 400, ikifuatwa na Barclays ambayo ilifuta wafanyakazi 301.

Benki ya Standard Chartered ilifuta kazi watu 300 na KCB ikatimua wafanyakazi 223. Benki zingine ni National (150), First Community (106), Sidian (108) na NIC (32).

Inaaminika huenda idadi ya waliofutwa kazi ni kubwa zaidi kwani baadhi ya benki hazikutoa takwimu zao.

Kulingana na ripoti hiyo, benki zilichukua hatua hii kutokana na hali ngumu ya kibiashara iliyosababishwa na sheria mpya iliyopitishwa mwaka wa 2016 ambayo iliondolea mabenki uhuru wa kuamua kuhusu riba wanayotoka kwa mikopo ya wateja wao.

“Mabenki yalichukua hatua kwa lengo la kulinda maslahi yao ya kibiashara katika mandhari magumu. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni kufuta watu kazi, kufunga matawi, kubadilisha masaa ya kufanya kazi au hata kuuza mabenki yenyewe,” ikasema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.