Wasiwasi wa makuli, madereva

Wahofia kazi yao itatwaliwa na SGR

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - WINNIE ATIENO na BRIAN OCHARO

WASIWASI umeanza kuwaingia madereva na makuli ambao hufanya kazi katika bandari ya Mombasa kutokana na mpango wa serikali ambao utapelekea reli ya kisasa ya SGR kubeba mizigo moja kwa moja kutoka kwenye meli.

Kwa sasa kazi hiyo hufanwya na madereva wa malori na makuli ambao hupakua na kupakia mizigo bandarini hadi kwa SGR.

Maafisa wa kutetea maslahi ya makuli, ambao hawakutaka kunukuliwa, walisema wanahofia huenda wakapoteza ajira endapo reli hiyo itaunganishwa na gati na kubeba mizigo moja kwa moja.

“Hatutaki kuonekana tunapinga mradi huo, lakini tuna wasiwasi kwani jambo hilo likifanyika tutakosa kazi. Kama reli itabeba mizigo moja kwa moja kutoka kwenye meli kazi ya makuli na madereva itakuwa gani?” akauliza afisa huyo anayefanya kazi bandarini.

Reli ya kisasa ya SGR inatarajiwa kukamilika Agosti ambapo

mizigo itabebwa moja kwa moja kutoka kwa meli.

Kwa sasa lori hutumika kusafirisha mizigo kutoka kwenye meli hadi katika reli ya SGR na kusafirishwa hadi jijini Nairobi.

Lakini shughli ya kurefushwa kwa reli hadi bandarini ambayo inakadiriwa kukamilishwa Agosti mwaka huu itawaacha mamia bila ajira.

Meneja wa SGR, Bw Maxwell Mengich, alisema ujenzi wa reli hadi katika mahali pa meli kutia nanga na kukaa gatini bandarini itarahisisha mizigo kubebwa moja kwa moja kutoka kwenye meli hadi katika SGR.

“Reli hiyo ikimalizwa kujengwa SGR itakuwa ikisafirisha mbolea, nafaka, miongoni mwa mizigo nyingine. Kwa sasa tuko asilimia 50 ya ujenzi huo,” alisema Mkurugenzi mkuu wa shirika la Reli nchini, Bw Atanas Maina.

Ujenzi huo umekadiriwa kugharimu Sh327 bilioni.

Alisema kuunganishwa kwenye milango nambari 11 na 21 kutaboresha utendakazi katika bandari, kando na kuleta mapato.

Picha/laban Walloga

Shehena ya kampuni ya usafirishaji mizigo ya Maersk ikiwa imebebwa na SGR kutoka bandari ya Mombasa hadi Nairobi juzi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.