Jombi ajuta kuvuruga starehe ya walevi kwa mahubiri

Taifa Leo - - Dondoo! Za Hapa Na Pale - Na John Musyoki

JOMBI mmoja mtaani hapa alifurushwa kikaoni kwa kutaka kuwahubiria walevi. Inasemekana jamaa alikuwa mraibu wa pombe aliyejulikana kijijini lakini akaamua kuokoka ijapokuwa wenzake hawakufahamu alikuwa amemkubali Yesu.

Siku ya tukio walipokuwa mangweni, jombi alifika na kuanza kushauri wenzake waache pombe na kutafuna miraa. “Nawasihi muache tabia ya kulewa na kutafuna matawi. Mimi nilikuwa mraibu wa pombe na kahaba lakini niliamua kuokoka. Ningependa kuwahubiria muache uraibu huu,” alisema.

Wenzake walianza kumfokea huku wakimlaumu kwa kuwaharibia starehe zao. “Eti unasema uliokoka wewe? Hatukuamini na hauwezi kutuhubiria. Kwenda kabisa hatutaki mahubiri yako.” walimzomea vikali.

Hata hivyo jamaa alikaa ngumu na kukataa kuondoka kikaoni. “Hakuna mtu wa kunifurusha hapa. Nina haki ya kusema chochote na kushuhudia mema aliyonitendea Mwenyezi Mungu,” alisema. Hali ilizidi kuchacha hadi ikabidi makalameni hao kuwa wakali zaidi na kutisha kumpiga. Jamaa alipoona ni kubaya aliamua kuuma kona huku akipiga nduru kuomba usaidizi.

Inasemekana baada ya kalameni kumfurusha waliamua kutomshirikisha katika mambo yao.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.