Hoja ya kuondoa hitaji la ada ya vyeti iungwe na wote

Taifa Leo - - Baruuajumbe - Na FAUSTINE NGILA

KWA muda mrefu, vijana nchini wamekabiliana na vizingiti wakati wa kusaka ajira, licha ya kuhitimu elimu ya chuo kikuu au ya taasisi za mafunzo.

Vijana hawa huhitajika kulipia vyeti kadhaa ili kukubalika kuingia kwa orodha ya watu wanaotakikana kujaza nafasi mbalimbali za kazi.

Wanahitajika kulipia vyeti vya nidhamu, vyeti vya kuthibitisha wamelipa mikopo ya Bodi ya Elimu ya Juu (HELB), vya maadili, vya kuashiria hawajakaidi kulipa mikopo na pia kuonyesha wanalipa ushuru.

Lakini wiki iliyopita, Bunge la Kitaifa lilipitisha hoja inayopendekeza kupiga marufuku mtindo wa kuwatoza ada vijana ili kupata vyeti hivi.

Hoja iliyobuniwa

Katika hoja iliyobuniwa Mwakilishi Mwanamke Nyandarua, Bi Faith Gitau,

kijana wa umri kati ya 18 na 35 anayesaka ajira hana pa kupata jumla ya Sh4,500 za kulipia vyeti hivyo muhimu.

Mbunge huyo alihoji kuwa vijana wengi wanaohitimu vyuoni wamelelewa katika familia zisizo na uwezo wa kifedha, na kuwaitisha hela

na wa za vyeti ni sawa na kuwaadhibu.

Tayari vijana hawa hupitia changamoto zingine kama ubaguzi wa umri na ukosefu wa uzoefu wakati kampuni na mashirika mengi yanapoajiri wafanyakazi wapya, na hivyo hawafai kuhangaishwa zaidi kwa kulazimishwa kutafuta pesa za kulipia ada ili vyeti vyao vikubalike.

Nasema hongera kwa Bi Gitau kwa kuwazia hoja hii na kuiwasilisha bungeni, kwa kuwa itaokoa maelfu ya vijana mijini ambao kikwazo pekee cha kupata kazi ni kutakiwa kulipa hela hizo, ambazo tayari hawana.

Ikiwa nchi hii inatazamia uchumi wake kuzidi kuimarika katika vizazi vijavyo, basi visiki vyote vinavyozuia ukuaji hasa kupitia kwa nguvukazi ya vijana vinafaa kuondolewa.

Utakuwa mwamko mpya ikiwa serikali itawapa vijana vyeti hivyo bila malipo, maanake hali hiyo mwanzo itapunguza ukosefu wa ajira miongoni mwao huku vizazi vijavyo vikipata wataalamu wa kukifaa kiufundi na kitaaluma miongo ijayo.

Hoja hii inapaswa kuungwa mkono na sekta zote za uchumi, wananchi na mashirika ya kijamii hadi hatua ya mwisho ya kutiwa saini na Rais. MWANDISHI

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.