Korti yamhukumu mshairi miaka 3 jela kwa ‘uchochezi’

Taifa Leo - - Habari Za Afrika Na Dunia - Na Mashirika

MAHAKAMA moja katika Jamhuri ya Somaliland imemhukumu mshairi mmoja mchanga miaka mitatu gerezani kwa madai ya “kuuchochea umma.”

Mshairi huyo, Nacima Qorane, alipatikana na hatia hiyo kwa kutunga shairi ambalo linashinikiza kuungana kwa taifa hilo na Somalia.

Upande wa mashtaka ulisema kwamba “aliikosea heshima” jamhuri hiyo kwa kuudhalilisha utawala wake. Katika shairi hilo, Bi Qorane alishinikiza kuungana kwa jamhuri hiyo na Somalia.

“Ameikosea heshima serikali kwa kuitukana kiwazi katika shairi hilo,” ukasema.

Hata hivyo, Kituo cha Kutetea Haki za Binadamu nchini humo kiliiomba serikali kumwachilia Bi Qorane na kuheshimu haki zake.

Mkurugenzi wa kituo hicho, Guleid Ahmed Jama, alisema kwamba “wanasikitishwa sana na hukumu hiyo.”

“Uhuru wa kujieleza umelindwa na katiba ya nchi yetu. Tunaiomba serikali yetu kuiheshimu katiba,” akasema.

Mbali na mshiri huyo, baadhi ya wasanii na wanahabari wamekamatwa na kuzuiliwa kwa madai kama hayo.

Somaliland ilitangaza uhuru wake mnamo 1991, ingawa haijatambuliwa kimataifa.

Bi Qorane alikamatwa mnamo Januari baada ya kurejea nchini humo kutoka mjini Mogadishu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.