Shujaa yaelekeza hasira zake katika Singapore 7s

Taifa Leo - - Spoti - Na GEOFFREY ANENE

BAADA ya kampeni yake ya kushinda medali kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola kugonga mwamba nchini Australia wikendi, Shujaa sasa inaelekeza nguvu zake katika kurejesha taji la duru ya nane ya Raga ya Dunia nchini Singpore.

Kocha Innocent Simiyu anatarajiwa kufanya badiliko moja la lazima katika kikosi chake kabla ya ziara ya Singapore hapo Aprili 28-29 baada ya mchezaji wa KCB, Arthur Owira kuvunjika mguu katika mechi ya makundi dhidi ya Zambia mjini Gold Coast, Australia. Nyota Collins Injera, Samuel Oliech na William Ambaka walipata majeraha madogo.

Owira alichezea Shujaa kwa mara ya kwanza kabisa katika duru ya pili ya Raga ya Dunia msimu huu nchini Afrika Kusini hapo Desemba 9-10, 2017.

Alifanyiwa upasuaji Jumapili na anatarajiwa kurejea Kenya hapo Alhamisi. Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) limesema kwamba kizibo cha Owira kitajulikana kesho.

“Bado tunasubiri Simiyu ataje mchezaji anayetaka ajaze nafasi ya Owira. Tutafichua jina la mchezaji huyo Jumatano. Tunafanya mpango wa kusafirisha mchezaji atakayetajwa hadi nchini Singapore kufikia Ijumaa,”

Mkurugenzi wa Raga wa KRU, Thomas Odundo alisema jana.

Aliongeza, “Simiyu amekuwa akinoa kikosi cha wachezaji 21 mazoezini kwa hivyo mchezaji yeyote atakayemchagua ndiye tutampeleka Singapore.”

Nchini Singapore, Kenya imetiwa katika kundi ngumu. Mabingwa wa Singapore Sevens mwaka 2016 Kenya watakabiliana na washindi wa Kombe

la Dunia mwaka 1993 Uingereza, mabingwa wa Las Vegas Sevens Marekani na mabingwa mara mbili wa Bara Ulaya, Ufaransa katika Kundi B.

Mara ya mwisho Kenya kukutana na Uingereza na Ufaransa ilikuwa katika duru ya Vancouver, Canada hapo Machi 10-11. Shujaa ililima Ufaransa 14-7 katika mechi ya makundi na kupepeta Uingereza 12-0 katika robo-fainali.

Picha/afp

Eroni Sau (kushoto) wa Fiji amkabili Nelson Oyoo katika mechi ya fainali ya Raga ya Dunia, duru ya Hong Kong mnamo Aprili 8, 2018.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.