Ameingia Kenya majuzi tu ila ana ndoto ya kuinua soka nchini

Taifa Leo - - Spoti - Na IGNATIUS OUNDO

Idadi ya wachezaji chipukizi kutoka mataifa ya kigeni kama vile Sudan, Rwanda, Kongo na kadhalika inazidi kuongezeka hapa Kenya.

Hali hii huenda ikainua viwango vya mchezo wa soka nchini iwapo vijana hao wataangaziwa mapema na kusaidiwa kukuza vipawa vyao kwa kujumuishwa katika klabu mbalimbali za mashinani na hata za ligi.

Malek Ghai, 13, ni mmoja wa chipukizi hao wanaoinuka kwa kasi katika kandanda. Kijana huyu mwenye asili yake nchini Sudan Kusini ana kipawa cha kuonea gere. Ana azimio la kuzisaidia timu za

Kenya kufika mbali kwenye kandanda.

Kinda Ghai japo ni mchanga kiumri, kimo chake kirefu kila mara kimemchochea kuwazidi wachezaji wa vikosi pinzani kwa maarifa huku pasi safi na chenga za maudhi zikichangia utamu wa mchezo wake.

Aidha, alipotua Kenya miezi miwili iliyopita, aliamua kujiunga na klabu ya Metro City kwa lengo la kuendeleza kipaji chake ambacho kinaonekana kukua kwa kasi mno na hivyo anaamini jina lake litajulikana kote Kenya kutokana na mchezo wake wa kupendeza.

Kikosini mwa Metro

City anajulikana kama

‘Wanyama’ kwani mbinu anazotumia kuwaadhibu wapinzani zinafanana kama zile za kiungo shupavu Victor Wanyama mchezaji wa klabu ya Tottenham Hotspurs na timu ya Taifa Harambee Stars. Kijana huyu anasema alianza kucheza kandanda akiwa na umri wa miaka 10 katika klabu ya Newstars FC kutoka nchini Sudan. Ni kipaji ambacho anasema kilichochewa na mastaa wa soka ya Uropa kama vile Wayne Roonye mchezaji wa zamani wa Manchester United ila kwa sasa anachezea klabu ya Everton nchini Uingireza. “Niligundua kwamba ninayo talanta ya kusakata soka nilipotimu umri wa miaka kumi pekee. Muda mfupi baadaye niliamua kujiunga na timu ya Newstars kwa lengo la kusaka maarifa zaidi huku nikiendeleza kipaji changu,” asema chipukizi Ghai.

Anasema atazidi kufanya mazoezi kwa bidi ili kiwango cha mchezo wake kiweze kuvutia timu kibao za mashinani pamoja na kujiundia jina.

Aidha, Ghai anacheza kama kiungo katika timu ya Metro City kutoka mtaani Kayole, Nairobi.

Mbali na soka Ghai ni mwanafunzi wa darasa la sita ingawaje hadi kufikia sasa hajafaulu kujiunga na shule za Kenya, japo anaamini anatapata nafasi ya masomo kwenye mojwapo ya shule za hapa Kenya.

“Kabla ya kuja Kenya nilikuwa katika darasa la sita, kwa sasa masomo yangu yamesimama kwa sababu bado sijafanikiwa kupata nafasi ya kujiunga na shule yoyote ili niendeleze kisomo changu. Hata hivyo, ninayo matumaini kwamba nitafaulu kupata shule katika siku chache zijazo ili niendelea kupata elimu kama nilivyokuwa kule Sudan, Asema Ghai.

Malek Ghai mchezaji wa klabu ya Metro City akiwa mazoezini. Picha/ignatius Oundo

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.