Al Swafaa hawajafa moyo maadamu macho yao yako kwa ligi za juu

Taifa Leo - - Spoti - Na JOHN KIMWERE

BAADA ya kuteleza na kushindwa kuinasa tikiti ya kusonga mbele, Al Swafaa FC imeanza kujipanga kivingine. Sasa Al Swafaa FC imepania kujitolea kwa udi na uvumba kuhakikisha imebeba tikiti ya kupandishwa ngazi kushiriki kinyang’anyiro cha Nairobi West Regional League (NWRL) mwakani.

Al Swafaa FC sasa inatiwa makali na kocha mpya Charles ‘Stam’ Kaindi ambaye pia hufundisha Kenya Forest Service (KFS) inayoshiriki Ligi ya Taifa Daraja ya Pili. Aidha timu hii imenasa huduma za waliokuwa wanasoka wa Uweza Soccer Academy kwa mkopo.

“Bila shaka raundi hii tumepania kupigana kufa na kupona kuhakikisha tumeibuka mabingwa kwenye kampeni za kipute cha Ligi ya Kaunti ya tawi la Nairobi West la Shirikisho la Soka ya Kenya (FKF),” asema Kaindi.

Anaongeza ‘’Tumefungua kampeni zetu vyema mwaka huu, kwa kushinda mchezo mmoja na kutoshana nguvu patashika moja.’’

Anakiri kuwa wanatarajia kazi zito mbele ya wapinzani wao kwa kuzingatia timu zote zinataka kufanya kweli ili kufuzu kupandishwa ngazi msimu ujao. Kadhalika alidai wamepanga wachezaji wa kikosi hicho kuhakikisha wamefaulu kumaliza kileleni mwa judwali la mechi za mkumbo wa kwanza. Kocha huyo anaamini ndani ya kikosi chake anao wanasoka wazuri na watafanya kweli kwenye michuano ya mwaka huu.

Nahodha wake, Frederick Juma anadai wamesukudia kuzua ushindani tosha kutimiza azimio lao kuibuka kidedea mechi za Kundi ‘A’ ili kukutanishwa na bingwa wa Kundi ‘B’ katika fainali.

Kadhalika anakiri kuwa mbio za michezo ya mwaka huu inatazamiwa kushuhudia mtanange mkali shughuli anazoamini haitakuwa mteremko.

Kipute hicho kinajumuisha timu kama Kibagare City, Kipande FC, Zion Winners, Real Mathare, WYSA FC, Nairobi Sports House na Kangemi Patriots kati ya zingine. Timu hii inapitia pandashuka nyingi tangia

ibuniwe ambapo imekuwa vigumu kugharamia mahitaji ya usafiri, vifaa vya kuchezea na matibabu hasa wachezaji wanapoumia dimbani. Kadhalika, wengi hujikuta kwenye pagumu kwa kulemewa kugharamia karo ya shule ambapo hugeukia mmiliki wake naye kulazimika kunyoosha mikono kwa wasamaria wema.

Timu hii inajumuisha Innocent Serete, Elvis Otwere, Frederick Juma (nahodha), Anthony Munene, Brian Gikundi, Hassan Kazungu, Abdul Abubakar, Victor Musunji, Edward Kuremi, Storm Otieno, Anwar Noah na Alvin Trump. Wengine Zalvin Amor, Duncan Ochieng, Hillary Lusivale, Patrick Audi, Enoch Ouma, Sebi Dakar, Sydney Okwaro, Joseph Kasika, Francis Wanyama, Lawrence Otieno, Imran Ibrahim, Leonard Ochieng, Derrick Areri, Wycliffe Odhiambo na Daniel Onyango.

Kaindi anashauri wachezaji wanaokuja kwa jumla nyakati zote kutia bidii kunoa vipaji vyao ili wakikomaa kispoti waweze kuteuliwa kuzipigia vikosi zingine zinazoshiriki ligi za haiba ya juu nchini.

Kadhalika aliendelea kuwafahamisha kuwa soka imegeuka ajira kama nyingine.

Picha/john Kimwere

Wachezaji wa Al Swafaa FC inayoshiriki kipute cha Ligi ya Kaunti, tawi la Nairobi West la Shirikisho la FKF.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.