PSG waliza Monaco vikali na kutwaa taji

Taifa Leo - - Spoti - PARIS, Ufaransa

NYOTA Angel Di Maria na Giovani Lo Celso walifunga mabao mawili kila mmoja na kuiwezesha Paris Saint-germain (PSG) kusajili ushindi mnono dhidi ya watani wao wa tangu jadi katika soka ya Ufaransa, AS Monaco uwanjani Parc des Princes mnamo Jumapili usiku.

Kwa matokeo hayo PSG hatimaye wametia kapuni ubingwa wa Ligue 1 kwa mara ya saba na hivyo kukiweka kikosi hicho katika mabuku ya historia kwa kutia kibindoni jumla ya mataji matano ya soka ya Ufaransa chini ya misimu sita.

Chini ya mkufunzi Unai Emery ambaye kwa sasa anajiandaa kumpokeza mikoba kocha wa zamani wa Borussia Dortmund, Thomas Tuchel, PSG walikizamisha chombo cha Monaco kwa kuwafunga jumla ya mabao matatu chini ya dakika 27 katika kipindi cha kwanza.

Lo Celso aliwafungulia PSG ukurasa wa mabao kunako dakika ya 14 kabla ya kuzamisha kabisa chombo cha wageni wao kwa kufunga bao la tatu dakika ya 27 baada ya Edinson Cavani kuyafanya mambo kuwa 2-0 katika dakika ya 17.

Awali, winga Angel Di Maria alikuwa amezidisha masaibu ya Monaco ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 70 kwa kutikisa nyavu za mabingwa hao wa Ligue1 mnamo 201617 katika dakika ya 20 kabla ya kuongeza goli lake Fowadi wa PSG Edinson Cavani na wenzake washerehekea ushindi wao dhidi ya Monaco mnamo Jumapili na hivyo kushinda ubingwa wa ligi hiyo kwa mara ya saba. dakika 10 baada ya nyota mzawa wa Colombia, Radamel Falcao kujifunga katika dakika ya 76.

Machozi ya Monaco waliositisha ukiritimba wa PSG katika soka ya Ufaransa msimu jana, yalifutwa na mvamizi Rony Lopes dakika ya 38. Bao hilo lilikuwa la nane kwa Lopes kutikisa wavuni kutokana na msururu wa mechi nane zilizopita.

Wakijivunia tayari ubingwa wa League Cup walioutia kapuni kwa mara ya tano mfululizo msimu huu, PSG kwa sasa wanalenga kunyanyua jumla ya mataji matatu hasa ikizingatiwa kwamba wamefuzu pia kwa nusu-fainali za French Cup.

Isitoshe, wako pua na mdomo kuweka rekodi mpya kwa kukamilisha kampeni za msimu huu kwa alama nyingi zaidi baada ya kufikisha jumla ya pointi 96 katika msimu wa 2015-16.

Hadi kufikia sasa, PSG wanajivunia alama 87 kutokana na mechi 33 na huenda wakajizolea alama 15 zaidi kutokana na michuano mitano iliyosalia msimu huu.

PSG kwa sasa ndicho kikosi cha kwanza katika ligi tano kuu za bara Ulaya kufikisha zaidi ya mabao 100 msimu huu licha ya kuzikosa huduma za mafowadi wao mahiri, Neymar Jr na Kylian Mbappe kwa muda.

Hadi walipokomolewa na PSG, Monaco wanaonolewa na kocha Leonardo Jardim hawakuwa wamezidiwa maarifa katika mchuano wowote kati ya minane ya awali.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.