Mawakili wapinga NHIF kuitisha cheti cha ndoa

Taifa Leo - - Front Page - Na RICHARD MUNGUTI

CHAMA cha wanasheria nchini LSK jana kiliwasilisha kesi katika mahakama kuu kupinga agizo la bima ya kitaifa ya huduma za afya (NHIF) la kutaka thibitisho la ndoa.

LSK inasema kwamba agizo la NHIF kwamba lazima wawili wathibitishe wamefunga pingu za maisha na wanaishi kama mke na mume kabla ya kunufaika na huduma zake linakaidi na kukandamiza haki za wanachama wake.

Chama hicho kinaomba korti iharamishe agizo hilo kwamba ni ushahidi tu wa Afi-

daviti zilizotayarishwa na Mahakimu utakaokubalika kwamba “wawili wameonana na wanaishi kama mke na mume.”

Chama hiki cha kutetea mawakili nchini kimeishtaki NHIF pamoja na mkurugenzi wake mkuu kikidai agizo hilo limepotoka na ukiukaji wa hali ya juu wa haki za wanachama wake wanaolipa ada zao kwa bima hiyo.

“Naomba hii mahakama ifutilie mbali agizo hilo la NHIF la kutaka cheti cha ndoa kuthibitisha mke au mume wamefunga ndoa ndipo wafaidi kwa huduma za bima za NHIF,” anasema kinara wa LSK katika kesi iliyowasilishwa katika mahakama kuu ya Milimani jana. LSK inaomba mahakama ifutilie mbali kabisa agizo la NHIF kwamba “haitaki ushahidi wa Afidaviti uliopigwa muhuri na wakili kuwa ushahidi wa kutosha kuthibitisha wawili wameoana.”

LSK inasema uamuzi huo wa NHIF umepotoka kabisa na kwamba utamlimbikizia mahakimu kazi ikitiliwa maanani kwamba “kuna mrundiko wa kesi katika baadhi ya mahakama.”

NHIF imesema tu itakubalia cheti cha kufunga ndoa kilichotolewa na maafisa wanaotambulika kisheria kama vile Wasajili wa masuala ya ndoa kutoka afisi ya mwanasheria mkuu, kadhi, mapadri, makasisi au afidaviti zilizotayarishwa na mahakimu kwamba wawili ni mke na mume.

“Ikiwa agizo hili litatekelezwa mawakili watanyimwa kazi,” LSK chasema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.