IEBC yahitaji angalau 5 kufanya kazi, sheria yasema

Taifa Leo - - Buriani Matiba - Na VALENTINE OBARA

HALI ya sintofahamu imeibuka kuhusu uwezo wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuendeleza shughuli zake baada ya makamishna watatu, wakiongozwa na Naibu Mwenyekiti Consolata Nkatha Maina, kujiuzulu jana.

Tume sasa imebaki na makamishna watatu pekee kwani Dkt Roselyn Akombe alikuwa wa kwanza kujiuzulu kabla ya uchaguzi wa marudio wa urais uliofanyika Oktoba 26, 2017. Aliamini haingewezekana kusimamia uchaguzi huru na wa haki kutokana na mgawanyiko na vitisho vilivyokuwepo.

Bi Nkatha alijiuzulu pamoja na Bw Paul Kurgat na Bi Margaret Mwachanya, kwa madai kuwa Mwenyekiti, Bw Wafula Chebukati, ameshindwa kuiongoza na pia Tume si huru kwani imeingiliwa na watu wa nje.

Kulingana na Sheria ya IEBC (2011), tume huhitaji makamishna wasiopungua watano ili kufanya maamuzi ya kuendeleza shughuli zake.

Licha ya chaguzi ndogo zinazotarajiwa kufanyika, shughuli ya kupanga upya maeneo ya mipaka nchini inatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Kwenye taarifa iliyosomwa kwa niaba yao na Bi Mwachanya, watatu hao walidai maamuzi hufanywa bila ushauriano na stakabadhi za siri hufichuliwa kwa umma “kwa maslahi ya kibinafsi”, huku wakijitenga na uamuzi wa kumsimamisha kazi Afisa Mkuu Mtendaji, Bw Ezra Chiloba.

Haya yametokea wiki moja baada ya Bw Chiloba kuagizwa kwenda likizo ya lazima kwa miezi mitatu katika hali iliyoibua mgawanyiko upya kati ya makamishna.

“Kusimamishwa kazi kwa Afisa Mkuu Mtendaji wa tume ni suala zito ambalo halingeingizwa mkutanoni ghafla. Wakati huo huo, tume ilikuwa imepanga tarehe za mikutano yake. Mkutano uliofanywa Aprili 6 ulistahili kufanyika Aprili 12 wakati makamishna wote wakiwa nchini,” akasema Bi Mwachanya, ambaye alisemekana kuwa katika ziara ya nje ya nchi Aprili 6.

Hata hivyo, kisheria mwenyekiti wa IEBC ana uhuru wa kuitisha mkutano wakati wowote mradi tu idadi kubwa ya makamishna wakubali kuhudhuria.

Mkutano ulioibua utata majuzi ulihudhuriwa na makamishna watano ingawa ilisemekana Bi Maina aliondoka walipoanza kutofautiana.

Licha ya kulalamikia uongozi mbaya, Bi Maina alisema wanaamini uchaguzi wa mwaka uliopita haukuathiriwa na tofauti zao.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.