Ahepa kimada kuona mashemeji zake baa

Taifa Leo - - Dondoo! Za Hapa Na Pale - Na TOBBIE WEKESA

KALAMENI mmoja eneo hili alilazimika kumhepa kimada wake walipoingia baa na kukutana na mashemeji wake. Inadaiwa polo alichukua hatua hiyo akihofia kupewa kichapo na mashemeji.

Duru zinasema polo alikuwa ameandamana na mrembo kujiburudisha. “Ilikuwa ni kawaida yake kwenda baa hiyo na uburudika kwa vinywaji,” alisema mdokezi.

Inasemekana kabla hata ya kuketi, polo aliwaona mashemeji zake pembezoni wakiburudika. Polo aligeuka mara moja na kutoka nje bila kumueleza mrembo kilichokuwa kikiendelea. “Kwani umeona nini unageuka hivyo mara moja,” mrembo alimuuliza polo huku alimfuata nyuma.

Polo alimtazama kimada na kuahidi kukutana naye siku nyingine. “Hapa ni kubaya. Wale jamaa wameketi kwenye ile kona ni mashemeji zangu,” polo alimueleza kimada.

Kulingana na mdokezi, mashemeji wa polo walikuwa wameingia katika baa hiyo saa chache kabla ya jamaa na kimada wake kufika.

Penyenye zinasema siku kadhaa kabla ya tukio, polo alikuwa amekashifiwa na mashemeji zake kwa kutowajibikia familia yake. Madai ya jamaa yalimshangaza demu. “Na si uliniambia hujaoa? Mashemeji wametoka wapi tena!” kimada alimuuliza polo kwa mshangao.

Polo hakumjibu mrembo. Kwake usalama wake ulikuwa ni muhimu sana.

Kulingana na mdokezi kalameni alifululiza hadi kwake huku akimuacha kimada nje ya baa. “Ukitaka kurudi ndani ya baa wewe rudi peke yako. Mimi sitaki hadithi nyingi,” polo alimfokea mrembo huku akirukia pikipiki na kuondoka.

Haikujulikana ikiwa uhusiano wake na kipusa huyo ulidumu baada ya kisa hicho.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.