Nimeoa ila tatizo ni mpenzi wa zamani haniachi

Taifa Leo - - Fumbo & Falaki -

Shangazi pokea salamu zangu. Mimi nimeoa na ninampenda sana mke wangu. Lakini mwanamke aliyekuwa mpenzi wangu tukisoma chuo kikuu anaendelea kuniandama akisema bado ananipenda. Nifanye nini? Kupitia SMS

Hali kwamba ulichagua kuoa mke mwingine badala yake ni ishara kamili kuwa hakutosha kuwa mke wako. Sasa una mke na unafaa kutulia na kutunza familia yako. Huyo anayekufuata akijua una mke anataka kuvuruga ndoa yako tu na unafaa kumuepuka kabisa.

Je, niache mume huyu nduli niendee mzuri?

Nimeolewa kwa miaka kadhaa na mume wangu amekuwa akinidhulumu hata sina raha kabisa katika ndoa yangu. Kuna mwanamume aliyekuwa akinitaka hata kabla sijaolewa na bado ananipenda kwani hajaoa. Je, nitakosea kumuacha niliye naye nihamie kwake? Kupitia SMS

Msimamo wangu ni kuwa si vyema kwa mtu kuvumilia dhuluma na mateso katika ndoa. Kama miaka yote ambayo umeishi katika ndoa imekuwa ya mateso, hutakosea kuondoka kutafuta maisha yenye furaha. Hiyo ni haki yako.

Hataki wazazi wake wajue nina mimba

Vipi shangazi. Nina mpenzi na sasa nina mimba yake. Wazazi wangu wanamjua na pia wanajua nina mimba yake. Wazazi wake pia wananijua lakini ameaniambia hataki wajue kuhusu mimba hiyo eti atawaambia nitakapopata mtoto.

Je, anaweza kuwa na njama mbaya kwangu? Kupitia SMS Ni vigumu kujua kinachoendelea katika mawazo ya mtu na mara nyingi inabidi uamini anayokwambia kama huna ushahidi wa kuonyesha kuwa anakuhadaa. Uzuri ni kwamba wazazi wenu wanajua kuhusu uhusiano wenu kwa hivyo utakapopata mtoto hatakuwa na namna ya kukukana. Ushauri wangu ni kuwa uondoe shaka na kusubiri hadi wakati huo.

Simu zake kwa mume wa zamani zinanikera

Kwako shangazi. Nilioa mwanamke aliyekuwa ameolewa na mwanamume mwingine na wakazaa watoto wawili. Sasa mwanamume huyo amekuwa akimpigia simu mara kwa mara wanaongea na jambo hilo linanichafua roho. Je, hiyo ni haki? Kupitia SMS

Kwa kukubali umuoe, mwanamke huyo alionyesha kwamba aliachana na mume wake akakatiza kabisa uhusiano wao na ndiyo maana alirudi kwao na watoto wake. Ni makosa kwake kuendelea kuwasiliana na mume wake wa zamani akiwa kwako. Mwambie wazi kuwa jambo hilo linakuudhi na hutavumilia. Hata kama walizaa pamoja, watoto hao sasa ni wako kwani ni wewe unayegharamia malezi yao. Kama hataki mwambie arudi kwa mwanaume huyo.

Sijamkosea lakini anataka tuachane

Shikamoo shangazi. Kijana ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka mitano amenigeuka ghafla akitaka tuachane na sijamkosea. Inawezekana kuwa amepata mwingine? Kupitia SMS

Hatua yake hiyo inaweza kutokana na mambo mawili. Labda hisia zake kwako zimepungua na anahisi kuwa hataki tena kuendelea na uhusiano huo, ama amepata mwingine. Bahati mbaya ni kwamba kama ameamua kujiondoa katika uhusiano huo huwezi kumzuia.

Mtoto anataka kurudi kwangu ila wazazi wa mama yake hawataki

Hujambo shangazi. Nilikuwa nimeoa lakini nikaachana na mke wangu akarudi kwao na mtoto wetu. Ingawa sikuwa nimemlipia mahari, mtoto huyo amekuwa akitaka kuja kwangu tuishi pamoja lakini mama yake na wazazi wake wanamkataza. Nifanye nini? Kupitia SMS

Wewe na mke wako huyo wa zamani kila mmoja wenu ana haki juu ya mtoto huyo hata kama hukuwa umemlipia mahari. Hata hivyo, kama mtoto huyo hajahitimu miaka 18, hawezi kuachwa ajiamulie kuhusu ni nani anayetaka kuishi naye kwani kuna mambo mengi ambayo hawezi kuelewa. Mgogoro wa aina hii hasa husuluhishwa kisheria kupitia kortini, kwa hivyo unaweza kuchukua hatua hiyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.