Wagonjwa wapitia mateso mikononi mwa wahudumu

Taifa Leo - - Front Page - Na TOM MATOKE

WASIMAMIZI wa Hospitali ya Rufaa ya Kapsabet katika Kaunti ya Nandi wamejipata pabaya baada ya familia moja kudai mama mjamzito alifariki baada ya kusubiri kwa muda mrefu bila kuhudumiwa.

Familia ya Bi Irene Cherono Rotich, mama wa watoto watatu kutoka kijiji cha Kapsaos, eneo la Nandi Kusini ilisema alipelekwa hospitalini alipopata matatizo akiwa karibu kujifungua.

Awali, alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Nandi Hills, lakini alipelekwa kwa hospitali hiyo ya rufaa hali yake ilipodhoofika.

“Hakuna muuguzi aliyekuja kumhudumia alipolazwa kwa wodi ya kina mama kujifungua. Alifariki tukimuangalia. Tunataka haki kwa mke wangu na

mtoto,” mumewe marehemu, Bw Cyprus Kiprono Rotich alieleza. Aliongeza kuwa mtoto pia alifariki, hata baada ya kusubiri muda mrefu na kuwasihi wauguzi kumhudumia mke wake.

Familia nyingine pia inadai mama mjamzito aliyekuwa na maumivu ya uzazi, alikosa kushughulikiwa kwa siku tatu, na kuzaa mtoto aliyeathirika ubongo.

Bw Abdi Kiprotich alieleza Taifa Leo kuwa, alimpeleka mkewe hospitalini Aprili 29, akitarajia kuwa angeshughulikiwa hata baada ya kuwasihi wahudumu.

Hata hivyo, ingawaje mkewe alinusurika, mtoto alizaliwa akiwa ameathirika ubongo na aliwekwa hospitalini.

“Mke wangu aliishia kujifungua mtoto ambaye alikuwa ameharibika ubongo na kuwekwa kwa oksijeni. Kuna wakati walitaka kumtoa kwa oksijeni lakini nilikataa na wiki iliyopita mke wangu na mtoto waliruhusiwa kutoka hospitali ya Kapsabet,” alieleza.

Wakati huo, mke wake akiwa hajajifungua, alishangaa kwa nini alikuwa hashughulikiwi, walinzi wa hospitali walimtimua na kuwaita polisi.

“Daktari alituambia sisi si spesheli na kwamba kulikuwa na kesi nyingine nyingi kama zetu. Walituambia tusubiri,” alidai.

Kulingana naye, polisi walipofika hawakufurahishwa na jinsi wagonjwa walikuwa wakishughuliwa na kuwataka wauguzi wawahudumie, kabla ya kuondoka bila kumkamata yeyote.

“Ninadai haki na ninataka wahusika waadhibiwe,” alieleza.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.