Wanasiasa wakongwe waunga mkono kuundwa kwa chama kipya cha Pwani

Taifa Leo - - Front Page - Na KAZUNGU SAMUEL

WANASIASA wakongwe katika eneo la Pwani jana walifurahia mpango wa kuanzishwa kwa chama kipya cha Pwani.

Hata hivyo, walihimiza maoni ya wananchi yatiliwe maanani na kuzingatiwa zaidi kuliko hisia za kisiasa.

Wakiongozwa na aliyekuwa mwakilishi katika Bunge la Afrika Mashariki, Bw Mohamed Zubedi walipongeza hatua hiyo na kuitaja kuwa yenye lengo zuri.

“Hatua ya kuanzisha chama cha Pwani ni nzuri na ina malengo mazuri. Tutakapoongea kwa sauti moja, hilo litasaidia kukuza azma yetu na kuboresha misingi yetu ya kisiasa,” akasema mwanasiasa huyo mkongwe.

Aidha, Bw Zubedi alitaka malengo kamili ya Wapwani kuwa na chama yawekwe wazi ili kuvutia hisia na maoni ya kila mkazi wa eneo hilo.

“Yafaa tujue tunaanzisha chama hiki ili kutoa mwaniaji wa Urais kutoka Pwani au ni kuunda chama ili tuwe katika serikali ya muungano 2022,” akasema Bw Zubedi.

Naye Bw Said Hemed, aliyewahi kuwa mbunge wa Kisauni kwa miaka mingi, aliunga mkono hatua.

“Ninaunga mpango wa kuwa na chama cha Pwani. Migawanyiko haiwezi kutupeleka kokote,” akasema Bw Hemed ambaye pia aliwahi kuwa balozi wa Kenya nchini Saudi Arabia.

Wengine ni aliyekuwa mbunge wa Ganze Bw Katana Ngala. Kwenye mahojiano, Bw Ngala alisema hatua hiyo ni mwafaka lakini lazima iwe itachukuliwa na kuthaminiwa na kila mtu.

“Tunataka kusonga mbele kwa sauti moja kama Pwani na hilo ndilo ombi letu,” alisema. Naye Bw Francis Baya ambaye wakati fulani alihudumu kama mkuu wa mkoa alisema umoja huo ni muhimu na utainua eneo hilo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.