Rais aidhinisha sheria kukabili habari feki

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - Na CHARLES WASONGA

MSWADA kuhusu uhalifu wa mitandaoni uliotiwa saini jana na Rais Uhuru Kenyatta utadhibiti usambazaji habari feki huku ikipendekeza adhabu ya Sh5 milioni kwa watakaokiuka sheria hiyo. Sheria hii ambayo itaanza kutumika baadha ya kuchapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali pia inaharamisha tabia ya watu wengi kuwatusi wenzao kupitia mitandao ya kijamii.

“Mtu ambaye atachapisha habari au data za uwongo akitaka habari zichukuliwe kuwa kweli kwa ajili ya kupata manufaa ya kifedha, atakuwa ametenda kosa na ataadhibiwa kwa kutozwa faini isiyozidi Sh5 milioni au afungwe jela kwa kipindi kisichozidi miaka miwili, au adhabu hizo mbili,” kinasema kipengee cha nne cha sheria hiyo.

Sheria hiyo pia inapendekeza adhabu kali kwa watakaopatikana na hatia ya kuendesha ulaghai mitandaoni, tabia ya kufikia siri za serikali bila idhini, kwa lengo la kufaidi atakuwa ametenda kosa. Atakayepatikana na hatia atatozwa faini ya Sh10 milioni, au kifungo cha miaka ishirini jela. “Na wale ambao watapatikana na hatia ya kuchapisha picha chafu za kuonyesha uchi wa watoto watatozwa faini ya kima cha Sh20 milioni au kifungo kisichopungua miaka 25 gerezani au adhabu zote mbili,” kinasema kipengee cha 13 cha sheria hiyo.

Wanaolengwa ni wale ambao huchapisha picha hizo kupitia programu za kompyuta au wamehifadhi picha hizo kwenye kompyuta zao.

Mbunge maalum Godfrey Osotsi alisema sheria hiyo mpya itakomesha visa vya dhuluma na uhalifu mitandaoni.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.