Afisa wa polisi ajiua kwa risasi

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - Na Abdimalik Hajir

AFISA wa Polisi wa Utawala (AP) aliyekuwa akihudumu katika Kaunti ya Garissa, alijiua kwa risasi.

Afisa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Garissa, Bw Aron Moriasse alisema wanachunguza kisa hicho.

“Afisa huyo alikuwa peke yake na risasi iliyomuua ilitoka katika bunduki aliyokuwa amekabidhiwa rasmi. Hata hivyo, tunaendelea na uchunguzi ili kubaini kiini chake,” akasema Bw Moriasse.

Alisema risasi hiyo ilipitia sehemu ya chini ya kidevu ikapitia ubongoni na kutokea kisogoni. Afisa huyo alifariki papo hapo.

Mwendazake alikuwa miongoni mwa maafisa wa Kikosi cha Dharura (QRT) ambao wamekita kambi katika afisi ya chifu wa eneo hilo mjini Garissa.

Duru za kuaminika ziliambia Taifa Leo kuwa afisa huyo hakufurahishwa na uamuzi wa kumhamishia katika kituo kingine cha polisi kilichoko katika mpaka wa Kenya na Somalia.

Visa vya maafisa wa polisi kujitoa uhai vinazidi kuongezeka katika maeneo mengi ya nchi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.