Mwezi wa kujizuia mlo na mabaya na kukumbatia udugu

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti -

NI mwaka mwingine ambapo Mwenyezi Mungu ametujaalia kuuona tena mwezi mtukufu wa Ramadhan. Ni mwezi ulio na faida tele kwa waumini wa dini ya Kiislamu, na ndani yake, kuna ibada kubwa ya kufunga (saum). Kwa kuwa Uislamu na dini zote za Mwenyezi Mungu zinahusisha vitendo, saum ni mojawapo ya mambo matano yanayoufanya Uislamu wa mtu kukamilika. Kwa wasioelewa Uislamu, nitazitaja kwa ufupi nguzo (mambo yote matano) hizo. Ya kwanza ni kukiri kwa moyo na kutamka kwa ulimi kwamba hapama mola anayefaa kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu. Na kwamba Muhammad ni mjumbe wake. Msomaji, utagundua baadaye kwamba, huko kuamini Muhammad kuwa mjumbe wa Mwenyezi Mungu hakuishii hapo. Kuna mojawapo ya nguzo za imani ambapo Waislamu huamini Mwenyezi Mungu alituma mitume (wajumbe) wengi, japo waliotajwa kwa majina ni 25 wakiwemo Adam, Nuhu, Ibrahim, Musa, Daud, Yakubu na hata Issa (Yesu). Baada ya kukubali kuwepo kwa Mwenyezi Mungu na wajumbe wake, jambo la pili kwa Muislamu ni kuzingatia swala tano kwa siku. Kisha kuna kuwajali masikini na wasiobahatika katika jamii. Ibada hii ya kutoa inaitwa Zaka. Ni kutoa ambako kumewekewa viwango maalum kama ambavyo Wakristo huita fungu la kumi. Lakini kwa Waislamu, kuna asilimia inayotolewa kutokana na mali yaliyokusanywa kwa mwaka mzima. Jambo la nne linalomfanya mtu kuwa Muislamu wa kweli ni hii ibada ya kujinyima kwa mwezi mzima. Inada ya Saum huja mara moja kwa mwaka katika mwezi wa Ramadhani. Kufunga ni kufunga kula, kunywa na tendo la ndoa kuanzia alfajiri hadi jua linapotua jioni. Katika kufunga pia, mtu anapaswa kujiepusha na kudanganya, kufanya mzaha wa kuudhi wengine na hata kushiriki katika mazungumzo au vitendo visivyokuwa vya kumjenga kiroho. Ni ibada hii ambayo Waislamu wanaianza rasmi na inatarajiwa kudumu kwa kati ya siku 29 na 30. Kabla sijataja jambo la tano, ningependa kusema kwamba, tunatarajia kuendeleza ukumbi huu wa Nasaha za Ramadhani kwa muda huo wote. Tunakaribisha mada, maswali, mapendekezo na hata michango kuhusu ibada hii muhimu kwa Waislamu kote ulimwenguni. Tumeweka mwisho wa makala, utakavyowasiliana nasi. Lile jambo la tano ni kwenda kuutembelea mji wa Makka nchini Saudi Arabia kwa ibada ya Hajj, angalau mara moja maishani.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.