Gilbert Deya huru kwa dhamana ya Sh10 milioni

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - Na MAUREEN KAKAH

MHUBIRI mbishi Gilbert Deya, anayekabiliwa na mashtaka ya wizi wa watoto aliachiliwa kwa dhamana ya Sh10 milioni na mdhamini wa kiasi sawa baada ya upande wa mashtaka kukosa kumaliza kesi katika muda uliopatiwa na Mahakama Kuu.

Akimwachilia kwa dhamana, Jaji Luka Kimaru alisema Deya amewahi kukwepa mahakama awali na anaweza kutoroka na kwa hivyo alipaswa kuweka dhamana kubwa kortini.

Hata hivyo, Jaji alilaumu upande wa mashtaka kwa kukosa kumaliza kesi hiyo hata baada ya kuongezewa siku 90 zaidi.

“Mshtakiwa anafaa kupewa masharti makali ya dhamana ili asitoroke, ana historia ya kutoroka na kusema mabaya kuhusu mahakama,” alisema Jaji Kimaru.

Mwaka jana, Hakimu Mkuu Francis Andayi aliagiza Deya aachiliwe kwa dhamana ya Sh1 milioni. Hata hivyo, upande wa mashtaka ulilalamika na kupinga uamuzi huo katika Mahakama Kuu ukisema tabia ya mhubiri huyo inaashiria kwamba anaweza kutoroka.

Hivyo basi, uamuzi wa Jaji Kimaru ni pigo kwa upande wa mashtaka ambao ulitaka Deya kuzuiliwa rumande hadi kesi yake itakapoamuliwa. Hakimu Mkuu Adayi alikuwa amepatia upande wa mashtaka siku 120 kukamilisha kesi dhidi ya Mhubiri huyo na kuonya dhidi ya njama za kuichelewesha. Bw Deya amekuwa akizuiliwa katika jela la Kamiti tangu Agosti 4 aliporudishwa nchini kutoka Uingereza na kushtakiwa kwa wizi wa mtoto.

Upande wa mashtaka ulikuwa umefahamisha korti kwamba mhubiri huyo alikwepa kushtakiwa tangu 2005 na ilibidi usubiri kwa miaka 12 kumfikisha kizimbani kujibu mashtaka.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.