Wito majaji wasitumie uhuru wa mahakama kudhulumu umma

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - Na BENSON MATHEKA

MAJAJI wanafaa kutumia uhuru wa mahakama kwa hekima na sio kwa kudhulumu umma, rais wa Mahakama ya Rufaa Jaji William Ouko amesema.

Alisema ni kwa kudumisha maadili ya hali ya juu ambapo majaji watafanya umma kuwa na imani na mahakama.

Akiongea katika hafla ya kumuapisha Jaji Msimamizi wa Mahakama Kuu Lydia Achode, Jaji Ouko alisema ili kuhakikisha nguzo nne kuu za Rais Uhuru Kenyatta zimetimizwa, majaji wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuwatendea haki Wakenya.

“Kama majaji, tunajua kuna masuala ya maadili kutuhusu, tunafaa kutumia uhuru wa mahakama kusaidia Wakenya,” alisema Jaji Ouko.

Akiongea kwenye hafla hiyo, Mkuu David Maraga alimtaka Jaji

Achode kutumia wadhifa wake mpya Jaji kuimarisha imani ya umma katika mahakama.

“Tunachotarajia kutoka kwa wadhifa wake ni kuhakikisha utendakazi wa Mahakama umeimarishwa na kwamba Wanjiku anavuna matunda ya kazi utakayotekeleza,” alisema Jaji Maraga.

Jaji Achode alichaguliwa Aprili April 23 kwa kupata kura 43 miongoni mwa 80 na kuwashinda majaji Mary Kasango na Asenath Ongeri.

Alichukua wadhifa huo kutoka kwa Jaji Richard Mwongo ambaye kipindi chake cha kuhudumu kilikamilika mapema mwaka huu. Miongoni mwa majukumu yake yatakuwa ni kusimamia Mahakama Kuu na kuhakikisha kwamba shughuli zake hazitatiziki.

Atakuwa na mamlaka ya kuteua majaji wa kusikiliza kesi ikibidi kwa kushauriana na Jaji Mkuu au majukumu mengine atakayopatiwa na Jaji Mkuu.

Jaji Achode alipanda ngazi katika idara ya mahakama kutoka Hakimu katika mahakama ya Kericho mwaka wa 1986.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.