Coca-cola yaanzisha kiwanda kipya cha juisi

Kiwanda kiligharimu Sh7b na kilifunguliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta juzi mtaani Embakasi, Nairobi

Taifa Leo - - Riziki - Na LEONARD ONYANGO

WAKUZAJI wa matunda huenda wakapata afueni baada ya kampuni ya soda ya Coca-cola kuzindua kiwanda cha kisasa cha kutengeneza sharubati (juisi).

Kiwanda hicho kilichogharimu Sh7 bilioni kilifunguliwa rasmi Jumanne na Rais Uhuru Kenyatta mtaani Embakasi, Nairobi.

Kampuni ya Coca-cola hununua machungwa kutoka kwa wakulima wa humu nchini haswa kutoka Kaunti ya Murang’a.

Zaidi ya wakulima 30,000 wa matunda wa humu nchini wanatarajiwa kunufaika na kiwanda hicho.

Kiwanda hicho kina uwezo wa kutengeneza chupa 28,000 za juisi na kinalenga kuajiri wafanyakazi 1500.

Tofauti na vinywaji vinginevyo ambavyo huwekewa gesi za kuhifadhi, juisi zinazotengenezwa na kiwanda hicho kipya kitahifadhiwa kwa joto.

“Kiwanda hiki hutumia joto kuhifadhi vinywaji tofauti na viwanda vinginevyo nchini Kenya ambavyo hutumia gesi. Juisi inahifadhiwa ndani ya chupa ikiwa na joto jingi,” akasema Daryl Wilson, mkurugenzi wa Vinywaji vya Coca-cola Afrika (CCBA).

Hicho ndicho kiwanda cha kwanza kinachotumia teknolojia ya kuhifadhi vinywaji kwa joto bila kutumia gesi. Kiwanda hicho ni cha pili katika ukanda wa Afrika Mashariki baada ya kile kimejengwa na kampuni ya Coca-cola nchini Uganda.

Rais Kenyatta aliyekuwa ameandamana na naibu wake William Ruto alisema uwekezaji huo unasaidia mpango wake wa maendeleo wa kuinua sekta kuu nene ambazo ni ujenzi wa makao bora na bei nafuu, matibabu kwa wote, kuongeza ajira na viwanda.

Alikitaka kiwanda hicho kuhakikisha kuwa asilimia 40 ya kandarasi, haswa matunda, zinazotolewa na kiwanda hicho zinawaendea wasambazaji wa humu nchini.

“Kanuni kuhusu Sheria ya Utoaji Kandarasi zitachapishwa katika Gazeti rasmi la Serikali hivi karibuni. Kanuni hizo zitahakikisha kuwa asilimia 40 ya kandarasi zinaendea Wakenya,” alisema.

Picha/patrick Kilavuka

MUUZA vinyago katika Soko la Maasai jijini Nairobi awaonesha watalii bidhaa hizo akitarajia watanunua. Bei yavyo huanzia Sh1,000 kwenda juu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.