Ukataji miti waendelea japo marufuku ingalipo

Taifa Leo - - Front Page - Na WAANDISHI WETU

WAFANYIBIASHARA katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa wanazidi kukata miti licha ya marufuku iliyotangazwa na serikali Februari.

Wakazi wanaoishi karibu na misitu mingi eneo la Pokot Magharibi, Uasin Gishu na Elgeyo Marakwet walieleza kuwa wafanyibiashara hujificha na kuingia

misituni kisha kukata miti ili kuchoma makaa hasa saa za usiku.

Baadhi ya misitu inayolengwa ni Embobut, Lelan, Tapach, Tangasi, Kamatira, Sina, Kanyerus na Sawa, Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Pokot Magharibi Abdulahi Khaliff alisema kuwa alifahamu kuhusiana na suala hilo kutokana na malalamishi ya wakazi.

Alisema ameanzisha uchunguzi na watakaokamatwa watafikishwa mahakamani. Bw Khaliff alisema afisi yake ilipokea malalamishi kwamba baadhi ya wafanyikazi wa umma walnahusika katika ukiukaji huo kwa kutumia magari ya serikali kusafirisha mbao kutoka misituni.

“Tumepokea habari kwamba baadhi ya maafisa wanatumia magari ya serikali kusafirisha mbao kutoka misituni kupeleka maeneo yasiyojulikana huku wengine wakisafirisha makaa,” alisema Bw Khalif wakati katika hafla ya kuhimiza upanzi wa miti katika msitu wa Kaprech, Kapenguria.

Alisema bado marufuku ya kukata miti na kuchoma makaa inaendelea na kuongeza kuwa serikali imeruhusu ukataji miti katika mashamba ya kibinafsi pekee kwa idhini kutoka kwa machifu.

Afisa mkuu msimamizi wa misitu katika Kaunti ya Pokot Magharibi Allan Ongere alitaja eneo la Talau kama moja ya maeneo yaliyoathiriwa na ukataji huo.

Hali kama hiyo inashuhudiwa pia Nandi ambako wakazi walithibitisha kuwa ukataji wa miti unaendelea ndani ya baadhi ya misitu.

Wakati huo, wataalam wa mazingira walielezea hofu yao kuhusu uharibifu wa vyanzo vya maji kutokana na uharibifu wa misitu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.