Ugonjwa wafuata wakazi kambini

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - MOHAMMED AHMED na DIANA MUTHEU Ripoti ya ziada na Justus Ochieng

WAATHIRIWA 700 wa mafuriko wanaoishi kambini katika Kaunti ya Tana River wamekumbwa na ugonjwa wa kuendesha, magonjwa ya maambukizi ya ngozi na maradhi yanayohusiana na upumuaji.

Kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu, walioathiriwa ni wakazi wanaoishi katika kambi saba ambazo ni miongoni mwa kambi 100 zilizozinduliwa katika kaunti hiyo baada ya mafuriko kuanza karibu mwezi mmoja uliopita. Kambi hizo saba ni Bandi, Gadeni, Dhanisa, Dumi, Lango la Simba, Mitapani na Walkoni.

Meneja wa Msalaba Mwekundu eneo la Pwani, Bw Hassan Musa alisema watoto ndio walioathiriwa zaidi na maradhi hayo.

“Magonjwa haya yamesababishwa na maji wanayoyatumia na pia msongamano hapa kambini. Lakini tumeweza kutibu waloathirika,” alisema Bw Musa.

Afisa wa matibabu ambaye haruhusiwi kuzungumza na vyombo vya habari, alisema kuchafuliwa kwa maji na mafuriko kulichangia kuzuka kwa ugonjwa ya kuendesha.

“Watoto wengi wanakumbwa na baridi wakati wa usiku. Wengine wanapata Numonia, kikohozi na homa lakini tunapambana kuwatibu walioathiriwa,” alisema afisa huyo.

Kliniki moja eneo la Danisa ilifurika wagonjwa, hasa wanawake na watoto waliokuwa waking’ang’ania kupata msaada wa matibabu unaotolewa na maafisa wa matibabu wa Msalaba Mwekundu.

Waathiriwa waliiomba serikali ya Kaunti na pia ya Kitaifa kuwasaidia kupata matibabu ya haraka.

“Maisha yamekuwa magumu hapa. Watoto wetu wanateseka na bado tumeagizwa kukaa kwenye kambi kwa muda mrefu zaidi. Tunahitaji matibabu ya haraka ili kuwaokoa watoto wetu,” alisema Fatuma Harbute, ambaye mtoto wake alikuwa miongoni mwa wale waliotibiwa magonjwa ya ngozi. Serikali imeagiza watu kuhamia katika sehemu iliyoinuka, baada ya kutangaza kwamba huenda bwawa la Masinga likafurika.

Kwingineko mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya wasichana ya St Mary’s Lwak iliyoko eneo la Rarieda Kaunti ya Siaya, alizirai na kufariki katika hali ya kutatanisha. Mkuu wa polisi wa Rarieda (OCPD), Johanna Chebii, alisema mwanafunzi huyo, alizirai akianua nguo mwendo wa saa moja Jumanne jioni.

“Alikimbizwa hospitali ya Kaunti Ndogo ya Bondo ambapo iligunduliwa alikuwa amekufa,” alisema Bw Chebii.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.