Siku ya punda yaadhimishwa

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - Na KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa Lamu jana walijumuika na wengine ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Punda.

Hafla ya aina yake iliandaliwa katika kituo cha Huduma kwa Matibabu ya Punda mjini Lamu na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi.

Kulikuwa na mashindano mbalimbali, ikiwemo usafi wa punda, jinsi mwenye punda anavyomtunza na kudumisha mahusiano na mnyama wake. Pia kuliteuliwa punda mrembo zaidi.

Akizungumza wakati wa maadhimishohayo, Afisa Msimamizi wa Kituo cha Huduma za Matibabu ya Punda nchini, Bw Solomon Onyango, alisema madhumuni ya kuadhimisha hafla ya punda ulimwenguni ni kuhakikisha haki ya punda inaheshimiwa.

Alisema mara nyingi wamiliki wa punda wamekuwa wakikiuka haki za wanyama wao, ikiwemo kuwabebesha mizigo kupita kiasi pamoja na kukosa kuwapa lishe bora na usafi.

Bw Onyango aliwataka wakazi wa Lamu na Kenya kwa jumla kuheshimu punda wao ili wawafaidi zaidi.

“Punda ana haki na lazima haki hizo ziheshimiwe. Huwezi kumchukua punda wa kilo 150 ukambebesha kilo hizo hizo 150 au zaidi. Lazima abebe nusu ya uzito wake,” akasema Bw Onyango.

Daktari wa Punda katika Kaunti ya Lamu, Bw Felix Rachuonyo, aliahidi kwamba wataendelea kuhamasisha wakazi jinsi ya kutunza punda wao.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.