Serikali yafunga kesi ya mauaji dhidi ya nduguye Kabando

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - Na JOSEPH WANGUI

SERIKALI imefunga kesi ya mauaji inayomkabili ndugu ya aliyekuwa mbunge wa Mukurweini Kabando wa Kabando, Ceasar Thiari.

Bw Thiari ameshtakiwa kwa kumuua mama yao kwa kumkata kwa upanga miaka mitano iliyopita.

Amekanusha kwamba alimuua Bi Rose Wachera Mwangi aliyekuwa na miaka 70 mnamo Julai 27, 2014, nyumbani kwake katika kijiji cha Kaini, Mukurwe-ini Kaunti ya Nyeri.

Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 17 katika kesi hiyo wakiwemo majirani, maafisa wa polisi na mtaalamu wa akili.

Akifunga kesi katika Mahakama Kuu ya Nyeri jana, kiongozi wa mashtaka Bw Festus Njeru Njue aliambia Jaji Jairus Ngaah kwamba kuna ushahidi wa kutosha dhidi ya Thiari ambaye amekuwa rumande katika gereza la King’ong’o tangu kesi ilipoanza kusikilizwa.

“Kisa hiki kilitokea kati ya saa saba na nusu na saa nane mchana. Ushahidi unaonyesha kwamba kifo hakikuwa cha kawaida mbali kilisababishwa na vitendo vya mtu mwingine. Kifo kilisababishwa na mshtakiwa,” alisema Bw Njue.

Alisema anategemea ripoti ya mpasuaji wa maiti iliyowasilishwa kortini kama ushahidi.

“Inaonyesha (ripoti) kwamba marehemu alikatwa mara kadhaa. Shahidi ambaye ni jirani, aliambia mahakama kwamba alimsikia marehemu akiomba usaidizi na kisha akaenda katika boma na kumpata marehemu akitokwa na damu akiwa amekatwa shingo kwa upanga uliokuwa kando yake.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.