Polisi wakabiliana na wanafunzi baada ya mmoja wao kuuawa

Taifa Leo - - Habari Za Afrika Na Dunia -

MAKABILIANO yalitokea Jumatano kati ya wanafunzi wa vyuo vikuu na polisi nchini Senegal siku moja baada ya mwanafunzi kuuawa wakati wa maandamano kuhusu kucheleweshwa kwa marupurupu yao.

Mohamed Fallou Sene, 25, mwanafunzi wa mwaka wa pili aliuawa Jumanne baada ya polisi kuitwa kutuliza fujo katika Chuo Kikuu cha Gaston Berger kilichoko mjini Saint- Louis kaskazini mwa Senegal.

Mkuu wa Polisi Ibrahima Ndoye Jumatano alisema uchunguzi wa maiti ya Sene ulibaini kuwa “alifariki kutokana na majeraha ya risasi”.

Hata hivyo, afisa huyo hakusema ni nani alifyatua risasi hiyo huku akiwaambia wanahabari kwamba uchunguzi kuhusu kisa hicho utakamilishwa baada ya siku nne zijazo.

Kifo cha mwanafunzi huyo pia kilichochea maandamano ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Cheikh Anta Diop katikati mwa jiji la Dakar, wanafunzi wakiwarushia mawe polisi ambao walijibu kwa kuwafyatuliwa gesi ya kutoa machozi.

Majengo kadhaa ya kibiashara yaliporwa katika ghasia hizo, kulingana na shirika la habari la AFP.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.