Jombi asusia salamu za baba mzazi akidai mzee ana mikosi

Taifa Leo - - Dondoo! Za Hapa Na Pale - Na Dennis Sinyo

JAMAA wa hapa aliwashangaza wenzake alipokataa kumsalimia babake mzazi akidai ana mikosi.

Jamaa alikuwa na wenzake wawili wakitoka kwake kwenda kazini babake mzazi alipotokea langoni akitaka kumuona. Hata hivyo, alikataa kumgotea babake akisema mzee huyo alikuwa na bahati mbaya. Jamaa alidai kila mara akisalimiana na babake asubuhi, siku humwendea vibaya kazini.

Mzee huyo alijaribu kumsihi mwanawe wazungumze kuhusu dharura iliyompata bila mafanikio. “Jamaa aliingia kwenye gari lake na kisha kuondoka na wenzake huku babake akimtazama machozi yakimlengalenga,” alisema mdokezi.

Wenzake walipojaribu kumshawishi kumpa sikio baba yake, alitishia kuwaacha wachape mguu hadi kazini. Ilibidi mzee huyo kurejea kwake kwani juhudi za kuzungumza na mwanawe ziligonga ukuta.

Alidai kwamba mwanawe alikuwa amebadilika na kumea pembe tangu alipopata kazi. Licha ya jamaa kushauriwa kumtii babake ili asipate laana, alidai alikuwa amekomaa na kwamba hangeyumbishwa na vitisho vyovyote vya kupata laana.

“Kama ni laana wacha anilaani. Mimi siogopi chochote!” alisema jamaa huyo. Yasemekana tangu siku hiyo baba yake aliacha kuzungumza naye.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.