Muafaka wa Uhuru na Raila usiwe na nia fiche

Tangu wawili hawa kuafikiana, wengi wa Wakenya bado hawajui kilichoafikiwa

Taifa Leo - - Barua - Na BENSON MATHEKA

KUFIKIA sasa kila Mkenya anakubali kuwa muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga umeleta utulivu nchini. Kutokana na utulivu huo kuna matumaini ya Wakenya kuishi kwa amani, utangamano na uchumi kuimarika.

Ni mazingira mazuri ya serikali kuhudumia Wakenya na kutimiza ahadi ambazo viongozi wa Jubilee walitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita. Kwa viongozi wa Jubilee, muafaka huo utaipa serikali nafasi ya kuzingatia huduma kwa raia kuliko ghasia zilizoshuhudiwa kabla ya Rais Uhuru na Bw Odinga kuafikiana.

Wawili hao waliambia Wakenya kwamba waliamua kuzika tofauti zao ili waunganishe jamii zote nchini. Kulingana nao, walitambua kwamba tofauti na ushindani wa kisiasa wakati wa uchaguzi umenyima nchi hii maendeleo na kuipaka tope ulimwenguni. Kwa hilo, ninakubaliana nao mia fil mia.

Hata hivyo, ikizingatiwa kuwa nchi hii imeshuhudia kuvunjwa kwa mikataba mingi ya maelewano kati ya wanasiasa, kuna hofu kwamba huenda muafaka wa

viongozi hawa wawili una njama fiche, mbali na kuunganisha Wakenya. Kwanza, ni wazi kuwa ni maelewano kati ya wanasiasa wawili ambao walichagua washauri wao wachache. Pili, mazungumzo yao yalikuwa ya siri hadi Machi 9 waliposalimiana nje ya ofisi ya rais na kutangaza mwanzo mpya. Tatu, walifichua machache mno kuhusu waliyokubaliana na jinsi yatakavyowafaa Wakenya wote.

UWAZI

Kwa maoni yangu, uwazi unahitajika katika masuala yoyote yanayohusu nchi. Hata baada ya kuteua kamati ya watu 14 kuwasaidia kuendeleza waliyokubaliana, ukweli ni kwamba Wakenya wanakisia tu pale muafaka huo utakawaelekeza. Hata wanasiasa wa pande zote mbili wanaochangamkia muafaka huo hawana habari utakapowaelekeza. Wanachofanya ni kuunga tu bila habari kamili kuhusu kile Rais Uhuru na Bw Odinga walikubaliana.

Huenda kuundwa kwa kamati ya watu 14 ni shughuli ya uhusiano mwema tu. Ninahisi kwamba japo kusalimiana kwa viongozi hawa kulituliza nchi, kulikuwa kilele cha kukamilisha

mazungumzo yao. Furaha yangu ni kuona amani ya dhati nchini Kenya. Hili linawezekana ikiwa muafaka huo ulikuwa wa dhati. Kwamba lengo la viongozi hao wawili ni kuwaunganisha Wakenya, kumaliza utata katika uchaguzi, kupigana na ufisadi na kuheshimu utawala wa kisheria.

Yatakuwa makosa makubwa ikiwa kufuatia mwafaka huo, kashfa za serikali hazitafichuliwa, upinzani utakosa makali na kuacha kukosoa serikali. Yatakuwa makosa zaidi ikiwa upinzani utanyamaza serikali ikivunja haki za binadamu na kukandamiza masikini. Yatakuwa makosa ikiwa mapendekezo ya kamati ya watu 14 yatapuuzwa sawa na ya kamati na tume za awali.

Pande zote zinafaa kujitokeza na kuthibitishia nchi kuwa muafaka huo ulikuwa kwa manufaa ya Wakenya wote na si ya watu wawili pekee.

Narudia kwamba uwazi ni muhimu ikiwa muafaka huo ulilenga kufaidi Wakenya wakati huu na siku zijazo.

Picha/maktaba

RAIS Uhuru Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga wakihudhuria mchezo wa gofu awali baada ya muafaka kati yao.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.