Tujiandae kwa maradhi mijini iwapo taka hazitazolewa

Taifa Leo - - Barua - Na BERNARDINE MUTANU

TAKATAKA katikati mwa jiji la Nairobi ni kero kubwa si tu kwa wakazi lakini pia kwa watu wengine wanaozuru jijini.

Ukweli ni kwamba zaidi ya kuharibu sura ya jiji, takataka zinaweza kuwa kiini cha ugonjwa wa kipindupindu. Mkurupuko wa kipindupindu tayari umeripotiwa katika Kaunti ya Nairobi. Aidha, takataka huvutia wadudu kama vile mbu ambao wanaweza kuambukiza magonjwa kama vile malaria, homa ya dengue na chikungunya.

Pia, takataka zinaweza kuchafua maji na kusababisha homa ya matumbo na kuhara.

Ndiyo maana kuna haja kubwa ya kuondoa taka yote katika mitaa ya Nairobi na kwingine kwa sababu ni tishio la afya.

Ukweli ni kwamba Nairobi inanuka, si mitaani si katikati mwa jiji, ni mandhari ambayo hakuna mtu yeyote anayafurahia.

Hata hivyo, si Nairobi pekee, miji mingi nchini Kenya inanuka kwa sababu ya takataka ambazo hazizolewi.

Wakati mvua inaponyesha, takataka hiyo, ambayo mara nyingi huwa na viini vya magonjwa hatari, hubebwa na mikondo ya maji hasa wakati huu mafuriko yanapozidi kuripotiwa katika maeneo tofauti nchini.

Hii ina maana kuwa hivi karibuni utasikia ripoti za kipindupindu katika kaunti kadhaa, si tu Nairobi, Tana River na Kiambu.

Ni wakati kwa serikali za kaunti na serikali kuu kujiandaa vilivyo kukabiliana na hali hiyo ikiwa idadi kubwa ya wananchi waepushwe na maambukizi ya mkurupuko huo.

Ushauri

Lakini inafaa tujiulize, ni lipi rahisi, kuzuia au kutibu? Kama wasemavyo wazee ‘ni bora kuzuia kuliko kutibu’, hivyo serikali inafaa kukabiliana na kiini kamili cha mkurupuko wa kipindupindu, ambacho ni takataka zilizotupwa ovyo na nyingine ambazo hazizolewi.

Katika mitaa ya mabanda ambako huwa ni chimbuko la magonjwa kama kipindupindu, takataka huziba mitaro, hivyo maji hayawezi kupita huru. Aidha, katika baadhi ya maeneo, wakazi huwa hawajali jinsi ya kukabiliana na kinyesi, ambacho hubeba viini vya magonjwa kama kolera.

Katika baadhi ya mitaa ya mabanda, mifereji ya maji hupita takatakani na kuhatarisha zaidi maji yanayotumiwa na wakazi.

Rais Uhuru Kenyatta alipozindua shughuli ya kusafisha jiji la Nairobi juma lililopita. Kuna hatari ya kuibuka magonjwa taka zisipozolewa mijini.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.