Wilshere, Hart waachwa nje ya Kombe la Dunia

Taifa Leo - - Spoti - Na MASHIRIKA

UINGEREZA imeacha Joe Hart na Jack Wilshere nje ya kikosi chake kitakachoshiriki Kombe la Dunia mwezi ujao na kumpa kinda Trent Alexanderarnold nafasi ya kujionyesha katika kindumbwendumbwe hicho.

Kocha mkuu Gareth Southgate ameamua kufuata kanuni zake na kuchagua kundi la wachezaji 23 chipukizi, walio na msisimko na wanaoweza kucheza mifumo tofauti ya mechi, lakini walio na ujuzi mdogo katika mashindano makubwa.

Hart alikuwa kipa nambari moja wa Uingereza katika Kombe la Dunia nchini Brazil na pia kuidakia katika makala mawili yaliyopita ya Kombe la Ulaya. Miezi mitano iliyopita, Hart alikuwa bado anashikilia nafasi hiyo.

Hata hivyo, amerukwa na Jordan Pickford, Jack Butland na Nick Pope baada ya kufanya masihara mengi michumani na kupoteza nafasi hiyo alipokuwa akichezea West Ham kwa mkopo kutoka kwa Manchester City.

Naye Wilshere alipeperusha bendera ya Uingereza mara ya mwisho ilipobwagwa 2-1 na Iceland katika mechi ya raundi ya 16-bora ya Kombe la Ulaya. Amekuwa akisumbuliwa na jeraha katika klabu yake ya Arsenal. Badala yake, Southgate, ambaye amekuwa kitumia mifumo ya 4-3-3, 3-4-3 na 3-5-2 katika miezi 18 amekuwa na timu hiyo, atawategemea Jordan Henderson, Eric Dier, Ruben Loftus-cheek, Jesse Lingard na Fabian Delph kama vifaa mbadala katika safu ya katikati. Alexander-arnold, 19, alianza kuchezea timu ya watu wazima ya Liverpool miezi 17 pekee iliyopita. Anajiandaa kukabili gunge Cristiano Ronaldo katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid hapo Mei 26 na kisha ataelekea Kombe la Dunia nchini Urusi. Uingereza imekutanishwa na Ubelgiji, Panama na Tunisia katika Kundi G.

Kikosi cha Uingereza: Makipa - Jack Butland (Stoke), Jordan Pickford (Everton), Nick Pope (Burnley); Mabeki - Trent Alexander-arnold (Liverpool), Kieran Trippier, Danny Rose (Tottenham), Ashley Young, Phil Jones (Manchester United), Fabian Delph, Kyle Walker, John Stones (Manchester City), Harry Maguire (Leicester), Gary Cahill (Chelsea); Viungo - Eric Dier, Dele Alli (Tottenham), Jesse Lingard (Manchester United), Ruben Loftus-cheek (Chelsea), Jordan Henderson (Liverpool); Washambuliaji - Harry Kane (Tottenham), Jamie Vardy (Leicester), Marcus Rashford (Manchester United), Raheem Sterling (Manchester City), Danny Welbeck (Arsenal).

Picha/afp

Kiungo mahiri wa Arsenal, Mwingereza Jack Wilshere.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.