NI ATLETICO Harambee yapangiwa mechi kabambe za kujipima

Taifa Leo - - Spoti - Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya soka ya taifa, Harambee Stars itamenyana na Swaziland, Equatorial Guinea, India, Chinese Taipei na New Zealand katika mechi za kirafiki kati ya Mei 25 na Juni 10.

Vijana wa kocha Sebastien Migne wataalika Swaziland na Equatorial Guinea nchini Kenya hapo Mei 25 na Mei 28, mtawalia.

Kisha Harambee itazuru mji wa Mumbai kwa mashindano ya Hero Intercontinental Cup yatakayoleta pamoja Kenya, India, Chinese Taipei na New Zealand kutoka Juni 1-10.

Kenya inafahamu Swaziland, lakini ni mara ya kwanza katika historia yake kukutana na Equatorial Guinea, India, Chinese Taipei na New Zealand.

Mara ya pekee Kenya na Swaziland zimewahi kukutana ni mwaka 2013 mjini Kitwe nchini Zambia.

Kenya ilishinda mchuano huo wa Kombe la COSAFA 2-0 kupitia mabao ya Edwin Lavasta. Kenya haikusonga mbele kwa sababu ilimaliza Kundi B nyuma ya Lesotho na Botswana. Ilikabwa 2-2 na Lesotho na kuzabwa 2-1 na Botswana.

Kenya na Equatorial Guinea zilipanga kupimana nguvu Septemba 8 mwaka 2015, lakini mechi hiyo ikafutiliwa mbali.

Katika kipindi cha mechi za kimataifa kilichopita mwezi Machi, Kenya na Swaziland zilikuwa na masaibu sawa. Kenya ilikabwa 22 na Comoros na kulemewa 3-2 na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) nchini Morocco nayo Swaziland ikachapwa 3-0 na Zambia kabla ya kutoka sare tasa na Ushelisheli.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.