Mizigo kutoka nje kukaguliwa kwa makini zaidi

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - DIANA MUTHEU na WINNIE ATIENO

SERIKALI imetangaza kuwa mizigo yote iliyoagizwa kutoka nchi za nje itakaguliwa kwa kina, ili kuzuia kuingizwa kwa bidhaa bandia, za magendo na zisizofikia viwango vinavyohitajika.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Adan Mohammed katika maelezo alisema serikali itaweka tanuri ya kuchomea taka katika bandari ili kusaidia kuharibu bidhaa hizo bandia, za magendo na zisizofikia kiwango kinachohitajika.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Kudhibiti Ubora wa Bidhaa (KEBS), Bw James Ongwae alisema kuwa maafisa wake watakuwa katika kila mkango wa kuingilia Kenya ili kukagua mizigo.

“Utaanza kukagua bidhaa hizo leo. Bidhaa zisizofikia kiwango kinachohitajika zitaharibiwa. Pia tumeanza ukaguzi wa makasha yote yanayosafirisha mitumba (viatu na nguo). Tayari tumezuilia makasha mawili katika bandari ya Mombasa yanayosafirisha mitumba hizo. Bidhaa zote zilizoagizwa kutoka nchi za nje zinazopitia katika uwanja wa ndege wa Eldoret zitakaguliwa kwa kina,” akaonya.

Bw Ongwae alisema kuwa maafisa katika sekta hiyo tayari wana orodha ya wamiliki wa makasha 163 ambazo zina bidhaa bandia, zingine za magendo na zisizofikia kiwango kinachohitajika zinazogharimu Sh250 milioni.

Mnamo Jumatano, bidhaa katika makasha 10 yaliharibiwa ambapo yale mengine yataharibiwa pia. Bw Ongwae aliongoza maafisa wa KEBS kuharibu bidhaa zenye dhamani ya zaidi ya Sh15 milioni zilizoagizwa kutoka nchi za nje.

Bidhaa katika makasha hayo 10 yalikuwa miongoni mwa yale 163 zote zikigharimu Sh250 milioni.

Uharibifu wa bidhaa hizo katika kampuni ya kutengeneza simiti ya Bamburi Cement ni miongoni mwa jitihada za serikali za kukomesha uagizaji wa bidhaa bandia, za magendo na zisizofikia kiwango kinachohitajika.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.