Lengo kuu la kufunga ni kupata ucha Mungu

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti -

Kila ibada katika Uislamu ina lengo maalum, na lengo hilo huwa Mwenyezi Mungu Analieleza sambamba na amri ya ibada hiyo. Hivyo basi,lengo kuu la kufunga kwa Waislamu ni kuweza kuwa wacha-mungu kama Mwenyezi Mungu Anavyotueleza katika Qur’an kwenye aya ya 183 suuratul Baqara. “Enyi mlioamini, mmelazimishwa kufunga (swaum) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kuwa wacha Mungu”(q 2:183). Kufunga Ramadhani ni chuo (shule) ya kumfunza mtu ucha Mungu ili pindi swaum inapokwisha mja adumu katika twaa (ibada) ya Mwenyezi Mungu hadi Ramadhani nyingine. Ucha Mungu ni kumuogopa Mwenyezi Mungu kwa kujilinda na maasi na kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu katika kila nukta ya maisha yake toka anapoamka hadi anapojibwaga kitandani kwa ajili ya kulala tena. Khalifa wanne wa uislamu Ali ibn Abitalib (R.A) anatueleza kuwa ucha mungu ni mambo manne: - kumuogopa Mwenyezi Mungu, kufanya shughuli zako zote kama Mwenyezi Mungu Alivyotueleza katika Qur’an, kuridhika na kidogo na kujiandaa na siku ya malipo. Ukiwa na hayo mambo manne huo ndiyo ucha Mungu. Kumuogopa Mwenyezi Mungu ni kuamini kwamba yupo na anakuona katika kila ufanyalo,hivyo basi unalifanya kwa tahadhari ya hali ya juu ili usije ukamuudhi. Mcha Mungu ni yule anayeishi kwa mujibu wa Qur’an, matendo yake yanakwenda sambamba na maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu. Swahaba wa mtume Muhammad Ubay ibn kaab (R.A) anasema alipoulizwa na sayyidna Umar (R.A) juu ya ucha Mungu, akamuuliza sayyidna Umar (R.A), je umeshawahi kupita njia iliyo na miba? Akamjibu “ndiyo”. Ubay (R.A) Akamuuliza, “ulifanyaje?” Umar (R.A) Akamwambia “nilipandisha nguo zangu juu na kuzikusanya pamoja na kupita kwa uangalifu mkubwa ili nguo zangu zisijenasa kwenye miiba hiyo. Ubay (R.A) Akamwambia na huo ndiyo ucha mungu,kujilinda mja na dhambi za dunia hii,ili aweze kuitimiza safari bila mikwaruzo ya miiba ya dhambi. Hivyo basi hii ndiyo taqwa,na mwenye hayo yote kwa pamoja, huyo ndiye mcha Mungu. Na hii ndiyo sababu ya Mwenyezi Mungu Kutuamrisha kufunga ili tuweze kuyafikia haya, na kuongeza daraja ya mambo haya kila mwaka hadi kufikia daraja ya juu katika ucha Mungu.

Na KHAMIS MOHAMED

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.