Mshukiwa wa 8 kortini kuhusu shambulio jijini

Washukiwa 7 wameshashtakiwa kuhusu shambulio hilo la Bw Muriuki

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - Na RICHARD MUNGUTI

MSHUKIWA wa nane katika shambulizi la mfanyabiashara Bw Timothy Muriuki katika hoteli ya Boulevard Nairobi ambapo alinyang’anywa Sh100,000 alishtakiwa jana.

Bw Hussein Suleiman alifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku.

Alikanusha shtaka la kumnyang’anya kimabavu Bw Muriuki pesa na wakati wa kitendo hicho wakamuumiza.

Kiongozi wa mashtaka Bi Pamela Avedi hakupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

“Kuna kesi nyingine tatu zilizofikishwa kortini kuhusu shambulio hili la Bw Muriuki. Tayari washukiwa wengine saba wameshtakiwa. Kesi hii itaunganishwa na hizo nyingine tatu,” alisema Bi Avendi.

Bi Avedi aliambia mahakama kuwa katika kesi hizo nyingine washukiwa waliachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000.

Kiongozi huyo wa mashtaka alisema kesi hiyo itaunganishwa mnamo Mei 23, 2018.

Wakili Cliff Ombeta anayemtetea mshtakiwa aliomba korti baada ya kesi kuunganishwa upande wa mashtaka uagizwe umkabidhi nakala za mashahidi.

Bi Mutuku aliamuru Bw Suleiman aachiliwe kwa dhamana ya Sh200,000 sawa na washukiwa wale wengine walioshtakiwa awali. Aliamuru kesi dhidi ya Bw Suleiman iuanganishwe na zile

nyingine.

Mnamo Jumatano washukiwa watatu walishtakiwa kuhusiana na shambulizi hilo mbele ya hakimu mkuu Bw Francis Andayi.

Walioshtakiwa mbele ya Bw Andayi ni Mabw Benjamin Peter Mulinge, Bernard Onyango Otieno na Michael Banya Wathigo.

Kufikishwa kortini kwao kulitimisha saba idadi ya washukiwa walioshtakiwa kwa shambulio hilo miongoni mwao Bw Muriuki akiwamo Mbunge anayewakilisha Kenya katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Bw Simon Mbugua.

Walioshtakiwa kufikia sasa ni Mabw Mbugua, Mulinge, Otieno, Suleiman Wathigo, Antony Otieno Ombok almaarufu Jamal na Benjamim Odhiambo Onyango almaarufu Odhis na Brian Shem Owino.

Picha/paul Waweru

Bw Hussein Suleiman katika mahakama ya Nairobi alikoshtakiwa kwa kumshambulia na kumpora mfanyabiashara Timothy Kariuki Sh100,000 Aprili 30, 2018 jijini Nairobi. Alishtakiwa pamoja na wengine na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.